Wapalestina waandamana kupinga uamuzi wa kuodolewa bendera ya Palestina katika maeneo ya umma

Mamia ya Wapalestina wakazi wa Quds Mashariki huko Palestina wameandamana kulalamikia na kupinga agizo la waziri mpya wa usalama wa ndani wa utawala haramu wa Israel wa kuondolewa bendera ya Palestina katika maeneo ya umma.

Wapalestina hao wakiwa wamebeba mabango na maberamu walisikika wakipiga nara dhidi ya Israel na waungaji mkono wake na kusisitiza kwamba, wamesimama kidete na wataendelea kutetea haki za taifa lao madhulumu la Palestina.

Maandamano hayo yaliyohudhuriwa pia na wanaharakati mbalimbali yalishuhudia pia Mayahudi wa mrengo wa kushoto wakishiriki katika maandamano hayo na kusisitiza kwamba, wanapinga agizo la kuondolewa bendera ya Palestina katika maeneo yote ya umma.

Kundi la Kiyahudi la mrengo wa kushoto linalojulikana kama ‘Al-Huriyah Lil-Quds’ limeandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, ‘tumekuja na tunapunga mikono yetu’ likiashiria kupeperushwa bendera ya Palestina  katika maandamano hayo.

Itamar Ben-Gvir, waziri wa usalama wa ndani wa utawala wa Kizayuni wa Israel ambaye hivi karibuni aliuvamia Msikiti wa al Aqsa, ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu akilindwa kikamilifu na jeshi la utawala wa Kizayuni, alinukuliwa majuzi akitoa amri ya kuondolewa bendera ya Palestina katika maeneo yote ya umma, agizo ambalo limekabiliwa na malalamiko makali kutoka kwa Wapalestina.

Waziri huyo mwenye misimamo mikali na chuki dhidi ya Uislamu na Wapalestina alidai wakati wa kutoa agizo hilo kwamba, kupeperusha bendera ya Palestina maana yake ni kuunga mkono ugaidi.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *