Wapalestina wamwomboleza Rais Raisi, wasema aliunga mkono mapambano yao ya ukombozi

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imetuma salamu zake za rambirambi kufuatia kufa shahidi Rais Ebrahim Raisi wa Iran na wenzake katika ajali ya helikopta.

Hamas imebainisha “hisia za huzuni na uchungu pamoja na ndugu zao wa Iran na kutangaza mshikamano kamili na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika tukio hilo la kusikitisha.”

Taarifa hiyo imesema mashahidi hao, “walikuwa na misimamo ya heshima ya kuunga mkono kadhia ya ukombozi wa Palestina” na “mapambano halali ya taifa la Palestina dhidi ya utawala wa Kizayuni.”

Hali kadhalika Hamas imesema: Walifanya juhudi za dhati na kuonyesha mshikamano na eneo thabiti la Ukanda wa Gaza” na pia walijitahidi kukabiliana na uchokozi wa Wazayuni dhidi ya watu wetu wa Palestina.”

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Mahmoud Abbas naye ametuma “rambirambi za dhati kwa ndugu wa Iran” kufuatia kifo cha Rais Raisi na wale aliokuwa ameandamana nao.

Huko Yemen, Mohammed Ali al-Houthi, Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi, ametuma “rambirambi” zake kwa watu wa Iran na familia za maafisa waliokufa shahidi katika ajali hiyo.

Mohammed Abdulsalam, Msemaji wa Ansarullah ya Yemen, naye amesema kwamba kufariki dunia Rais Raisi “sio tu hasara kwa Iran bali pia ni hasara kwa ulimwengu wa Kiislamu, hasa kwa Palestina na Gaza.”

Harakati ya muqawama ya Hizbullah ya Lebanon pia imemtaja rais wa Iran kama “ndugu na muungaji mkono mkubwa’ wa harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu (muqawama) ya Lebanon.

Vile vile, Hizbullah imesema Amir-Abdollahian alikuwa muungaji mkono wa harakati za muqawama na alijitolea katika uungaji mkono huo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *