Wapalestina waunga mkono Timu ya Soka ya Iran kabla ya mchuano wa Kombe la Dunia na Marekani

Mashabiki wa soka wa Palestina wameonyesha uungaji mkono mkubwa kwa timu ya taifa ya kandanda ya Iran, iliyopewa jina la utani la Team Melli, kabla ya mechi muhimu ya Kombe la Dunia dhidi ya Marekani leo usiku.

Mashabiki wa soka wa Palestina na Iran walikusanyika katika hafla moja katika mji mkuu wa Qatar wa Doha, na kuinua bendera za mataifa hayo mawili.

Jumuiya ya Vijana wa Al-Quds ilisema kuwa uungaji mkono kwa Timu ya Taifa ya Soka ya Iran unakuja ndani ya fremu wa mshikamano wa Wapalestina na timu zote za kitaifa za Waarabu na Waislamu zinazoshiriki Kombe la Dunia la FIFA la 2022 kwa ujumla. Wapalestina wanasema mechi ya leo Jumanne ni muhimu zaidi ya zote kwani  kwa upande mmoja kuna Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo  ni  muungaji mkono mkuu wa taifa la Palestina, na upande wa pili ni Marekani ambayo ni mshirika na muungaji mkono mkubwa zaidi wa utawala haramu wa Israel unaozikoloni na kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.

Washiriki katika mjumuiko wa leo wameonyesha shauku kubwa huku wakiwa na mabango yaliyoandikwa kwamba al-Quds (Jerusalem)  ni mji mkuu wa milele wa Palestina na huu ni msimamo imara wa Wairani na Wapalestina.

Mashabiki wa Iran pia walipongeza msimamo wa Wapalestina wa kuunga mkono timu ya taifa ya nchi yao, na kujivunia umoja kati ya watu hao wawili.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *