Askari wa Jeshi la Uganda wamefanikiwa kuwaangamiza wanamgambo 15 wa kundi la waasi la ADF katika mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Hayo yalisemwa jana Jumanne na Kanali Deo Akiiki, Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Uganda (UPDF) katika mahojiano na gazeti la The East African na kuongeza kuwa, wapiganaji hao wa ADF waliuawa walipojaribu kuvuka Mto Semliki karibu na mpaka wa DRC.
Amesema baadhi ya waasi hao wa ADF waliuawa kwa kupigwa risasi, huku wengine wakifa maji mtoni wakijaribu kutoroka baada ya kushambuliwa na askari wa Uganda.
Kanali Akiiki amekanusha madai kuwa kuna idadi kubwa ya raia wameuawa na kujeruhiwa katika makabiliano hayo baina ya wanajeshi wa Uganda na wanamgambo wa ADF.
Onan Bagonza, Mwenyekiti wa Kaunti Ndogo ya Bweramule awali aliliambia gazeti la Monitor la Uganda kwamba, raia kadhaa wameuawa, huku mamia ya wengine wakiyakimbia makazi yao kutokana na mapigano hayo ya Jumatatu baina ya UPDF na waasi wa ADF.
Mwezi uliopita wa Oktoba, watu wasiopungua saba waliuawa katika shambulio la ADF mjini Maboya eneo la Beni katika mkoa wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kundi hilo la waasi linalotokea kaskazini mashariki mwa Uganda limekuwa likiendesha shughuli zake katika maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa DRC tangu muongo wa 90, ambapo limeua mamia ya watu, na kupelekea malaki ya wengine kuwa wakimbizi.