MASWALI yameibuka kuhusu hali ya kampeni za Azimio La Umoja huku washirika wa Rais Uhuru Kenyatta hasa kutoka eneo la Mlima Kenya na mashariki mwa nchi wakionekana kulegeza kamba katika juhudi za kumpigia debe mgombeaji urais wa muungano huo, Raila Odinga.
Hii ni baada ya wanasiasa wa chama cha Jubilee na washirika wake kutoonekana katika mikutano ya kampeni ambayo Bw Odinga alifanya wiki jana katika eneo la Magharibi isipokuwa aliyekuwa mbunge wa Gatanga, Peter Kenneth na aliyekuwa Mbunge wa Starehe, Maina Kamanda.
Viongozi wa chama tawala waliomsaidia Bw Odinga kupenya eneo la Mlima Kenya wakiwemo magavana Francis Kimemia wa Nyandarua, James Nyoro wa Kiambu na Lee Kinyanjui wa Nakuru hawajaonekana katika kampeni za Bw Odinga kwa muda sasa.
Bw Kinyanjui alisema, japo anaunga Azimio, anajenga chama chake cha Ubuntu Peoples Forum kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.
Kampeni za Bw Raila tangu aliporudi nchini kutoka ziara nchini Uingereza zimekosa sura ya muungano wa Azimio La Umoja huku zikionekana kuwa hafla za chama chake cha ODM.Duru zinasema kwamba, ushindani kwenye mchujo umesababisha baridi katika kampeni za Azimio huku vyama tanzu vikijipanga kivyao.
Baadhi ya vyama tanzu vya muungano huo vinalaumu ODM kwa kunyakua wanachama wake huku viongozi wa vyama wakijikuna vichwa kuhusu mchujo unaotarajiwa kukamilika Aprili 26.
Wanasiasa wa Mlima Kenya kama vile Mwakilishi wa Wanawake kaunti ya Murang’a Sabina Chege na mbunge wa Kieni Kanini Kega na Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni ambao walikuwa wakiandamana naye hawajaonekana katika mikutano ya kampeni ya Bw Odinga kama ilivyokuwa awali.
“Hakuna kiongozi wa Jubilee amehepa kampeni za Azimio ambacho ni chombo chetu. Tunajipanga kwa mchujo na tutarudi kwa kishindo hadi Raila aingie Ikulu,” alisema afisa mmoja wa chama hicho ambaye aliomba tusimtaje jina kwa kuwa sio msemaji wake.
Hawakushiriki kampeni
Ingawa viongozi wa vyama vingine 26 vilivyotia saini muungano huo waliahidi kumpigia debe Bw Odinga, hawajaonekana wakijiunga na kampeni zake katika ngome zao au kuandamana naye maeneo mengine.
Katika eneo la Magharibi, viongozi wa chama cha Democratic Alliance Party – Kenya (DAP-K) hawakushiriki kampeni za Bw Odinga za siku nne ambako ODM ilipokea wabunge na kuwapa tiketi za moja kwa moja.
Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na Gideon Moi wa chama cha Kanu ambao walikuwa wakisuka muungano wa One Kenya Alliance kabla ya kujiunga na Azimio kupitia Jubilee cha Rais Kenyatta hawajaonekana kwenye kampeni za Bw Odinga.
Mara ya mwisho Bw Kalonzo kuonekana hadharani akiwa na Bw Odinga ilikuwa kwenye kongamano la kitaifa la wajumbe wa chama cha Upia kinachoongozwa na Waziri wa Fedha Ukur Yatani.
Akizungumza katika kongamano hilo, Bw Musyoka aliahidi kumpigia debe Bw Odinga kuwa rais wa tano wa Kenya lakini akatoweka kwenye kampeni baada ya kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua ambaye alikuwa kinara mwenza wa OKA, kuingia Azimio.
Kabla ya Bw Musyoka kujiunga na Azimio, magavana watatu wa kaunti za Ukambani Alfred Mutua( Machakos) ambaye ni kiongozi chama cha Maendeleo Chap Chap, Charity Ngilu (Kitui) wa chama cha Narc na Kivutha Kibwana (Makueni) wa chama cha Muungano walikuwa msitari wa mbele kumpigia debe Bw Odinga eneo la Ukambani na maeneo mengine.
Hata hivyo, tangu Musyoka ajiunge na muungano huo, hawajaonekana pamoja kwenye mkutano wa kampeni.
Bi Ngilu ambaye ni mwachama wa bodi ya uchaguzi ya Bw Odinga aliandamana na kiongozi huyo wa ODM, Uingereza.