Wasiwasi wa kieneo na kimataifa kuhusu tabia ya ubaguzi wa rangi ya baraza jipya la mawaziri la Israel dhidi ya Wapalestina

Hatua ya hivi karibuni ya Waziri wa Mambo ya Ndani wa utawala haramu wa Israel, ya kuingia kinyume cha sheria katika Msikiti Mtukufu wa al-Aqsa imekabiliwa na radiamali kali ya kieneo na kimataifa, na ambayo imezipelekea nchi za China na Imarati kuomba kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kujadiliwa suala hilo.

Jumanne asubihi, Itamar Ben-Gvir, huku akiwa anasindikizwa na askari usalama ghasibu wa Israel na akiandamana na walowezi kadhaa wa Kizayuni, aliingia bila kujali lolote, katika msikiti wa Aqsa na hivyo kuuvunjia heshima wazi wazi.

Hiyo si hatua pekee ya uhasama ambayo imechukuliwa na baraza jipya la Benjamin Netanyahu dhidi ya Wapalestina katika siku za karibuni. Baraza hilo jipya lilianza kufanya kazi Alhamisi ya wiki lililopita. Ikiwa ni chini ya wiki moja vikosi vya utawala ghasibu wa Israel vimetekeleza mauaji ya Waplestina wasiopungua sita bila kuwajibishwa kisheria.

Hatua ya ubaguzi wa rangi inayotekelezwa na waziri wa mambo ya ndani wa utawala huo inathibitisha wazi kuwa utawala huo unaokalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina umeazimia kuzidisha jinai zake dhidi ya Wapalestina wasio na hatia, suala ambalo limeongeza wasiwasi wa mataifa ya eneo na kimataifa. Nchi za eneo zikiwemo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Saudi Arabia, Uturuki, Qatar na Imarati zimetoa taarifa tofauti zikilaani vikali hatua za ukatili zinazochukuliwa na serikali mpya ya Kizayuni dhidi ya Wapalestina.

Hio ndio maana nchi kama vile China na Imarati zimeitisha kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kujadiliwa suala hilo, ikiwemo hatua ya karibuni ya waziri wa usalama wa utawala huo ya kuuvunjia heshima Msikiti wa al-Aqsa. Wapalestina pia wanatumia uwezo wao wa kimataifa ili kufuatilia na kusimamisha mara moja jinai za utawala haramu wa Israel dhidi yao. Katika uwanja huo, Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amemtaka mwakilishi wa mamlaka hiyo katika Umoja wa Mataifa aanzishe mara moja juhudi za kulitaka Baraza la Usalama lichukue hatua za dharura kwa ajili ya kulilazimisha baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu zisimamishe haraka hatua zake za jinai dhidi ya Wapalestina.

Mashinikizo tofauti ya kieneo na kimataifa hatimaye yamempelekea Benjamin Netanyahu ambaye alikuwa amepanga kufanya safari yake ya kwanza nje ya utawala huo huko Imarati wiki ijayo akiwa waziri mkuu wa Israel katika kipindi hiki kipya, kuakhirisha safari hiyo hadi wakati usiojulikana.

Inaonekana kuwa mashinikizo ya ndani, kieneo na kimataifa dhidi ya baraza jipya la Netanyahu yanatokana na masuala mawili makuu. Suala la kwanza ni kuwa watu wote wanaamini kuwa baraza hilo linawajumuisha watu walio na misimamo mikali inayokiuka mipaka inayokubalika kimataifa na ambao wana rekodi mbovu ya kuhusika na uhalifu na jinai hasa ya ubaguzi wa rangi.

Sula la pili ni kuwa wachambuzi wa mambo na viongozi wa nchi nyingi duniani wanaamini kuwa hatua kama hizo za baraza jipya la Netanyahu zinaweza kuwa na matokeo mabaya na hatari sana kwa usalama wa nchi za eneo la Asia Magharibi. Akizungumza Jumanne usiku, Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Chama cha Hisbullah cha Lebanon ametaka kufutiliwa mbali serikali mpya ya Israel ambayo inataka kuushambulia mji mtakatifu wa Quds, na kutakadharisha kuwa kufanya hivyo si tu kutalipua hali ya mambo huko Quds na Palestina pekee bali katika eneo zima la Asia Magharibi.

Nukta ya kuzingatiwa hapa ni kwamba kiburi ambacho kimeupelekea utawala haramu wa Israel kuvamia na kuuvunjia heshima Msikiti Mtukufu wa al-Aqsa na kuongeza jinai zake dhidi ya Wapalestina kimechochewa pia na tabia pamoja na siasa za nchi za Kiarabu ikiwemo Imarati kuhusiana na utawala huo. Hata kama sasa Imarati imeomba kufanyika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kujadiliwa hatua za kijinai za utawala haramu wa Israel huko Quds, lakini ni wazi kuwa siasa zake za kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo unaokalia kwa mabavu Quds Tukufu, tangu miaka miwili iliyopita, ni moja ya sababu ambazo zimeushajiisha na kuufanya upate kiburi cha kudumisha jinai zake dhidi ya Wapalestina bila kuogopa lolote. Kwa maneno mengine ni kuwa hatua ya kijinai iliyochukuliwa hivi karibuni na Itamar Ben-Gvir Waziri wa Mambo ya Ndani wa Utawala ghasibu wa Israel katika kuuvunjia heshima Msikiti Mtukufu wa al-Aqsa ni moja ya matokeo ya moja kwa moja ya tabia na siasa za Imarati za kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo wa kibaguzi.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *