Ziara ya hivi karibuni ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron barani Afrika haikifaulu.
Hayo ni kwa mujibu wa wataalamu kadhaa wa masuala ya Afrika na wanaharakati wa mashirika ya kiraia.
Wiki iliyopita, Macron alitembelea Gabon, Angola, Jamhuri ya Kongo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ikiwa ni katika jitihada zake za kuhuisha satwa ya Ufaransa katika nchi hizo.
Akiwa Gabon, Macron alitangaza “mwisho wa sera ya Francafrique,” ambayo ni sera ya satwa ya Ufaransa katika koloni zake za zamani barani Afrika.
Macron alidai kwamba Paris ni “mpatanishi asiyeegemea upande wowote ambaye jukumu lake si kuingilia siasa za ndani.”
Mwanaharakati Cheikh Fall akizungumza na shirika la habari la Anadolu amesema kwamba Macron anaendelea kuidharau Afrika, na kuongeza: “Ikiwa Macron angetoa kauli hiyo ya ‘Francafrique imekwisha’ mwishoni mwa ziara yake, baada ya kukutana na viongozi wa Afrika, inaweza kuwa na maana. Kauli hiyo imejaa dharau na kiburi.”
Fall, ambaye ni mwanzilishi wa vuguvugu la kiraia la AfricTivistes, amesema wito wa Afrika kuwa na uhuru kamili ulimlazimu Macron kufanya ziara hiyo.
Abdennour Toumi, mtafiti katika Kituo cha Mafunzo ya Mashariki ya Kati (ORSAM, Türkiye), amesema Macron bado anaona Afrika kama uwanja wake wa kujifaragua na kufanya inavyotaka.
Toumi amesema ziara ya hivi karibuni ya Macron barani Afrika “imefeli kabisa,” na kuongeza kuwa: “Paris lazima irekebishe sera yake ya Afrika kwa kuwa hisia dhidi ya Ufaransa ni kubwa sana barani humo. Leo hii, vijana wa Kiafrika hawaitegemei Ufaransa tena, wana machaguo mengine.”
Toumi pia amesema kuwa mataifa ya magharibi na kati mwa Afrika, pamoja na ukanda wa Sahel, hayataki kuingiliwa na Ufaransa na yanataka kuheshimiwa.