Watoto 6 ni katika Wapalestina 24 waliouliwa kikatili na Wazayuni tangu Ijumaa

Idadi ya Wapalestina waliouliwa shahidi katika jinai zinazoendelea za utawala wa Kizayuni huko Ghaza imeongezeka na kufikia watu 24 wakiwemo watoto wadogo sita.

Utawala katili wa Israel unaoua watoto wadogo bila kiwewe, ulianzisha mashambulizi makubwa juzi Ijumaa dhidi ya maeneo ya makazi ya watu huko Ghaza na hadi leo Jumapili, mashambulio hayo yanaendelea.

Wizara ya Afya ya Ukanda wa Ghaza imesema kuwa, idadi ya Wapalestina waliouwa shahidi walikuwa ni 24 wakiwemo watoto wadogo 6 na wengine 215 walikuwa wamejeruhiwa hadi wakati inatangaza habari hiyo.

Kwa upande wake, harakati ya Ansarullah ya Yemen pamoja na jeshi la nchi hiyo wamesema kuwa, wanasubiri amri tu kutoka kwa viongozi wao, ili waingie vitani kulisaidia taifa la Palestina na kukilinda Kibla cha Kwanza cha Waislamu yaani Msikiti wa al Aqsa.

Televisheni ya Al Masirah imemnukuu Brigedia Jenerali Yahya Saree, msemaji wa majeshi ya Yemen akisema mapema leo Jumapili asubuhi kuwa, vikosi vyote vya ulinzi vya nchi yake likiwemo jeshi na kamati za kujitolea za wananchi wa nchi hiyo, viko tayari kulihami kijeshi taifa la Palestina wakati wowote itakapolazimu kufanya hivyo.

Makundi ya mapambano ya Kiislamu ya Palestina nayo yanaendelea kujihami kwa kuyatwanga kwa makombora na maroketi maeneo ya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni na ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel.

Hata mji mkuu wa utawala wa Kizayuni, yaani Tel Aviv haujasalimika na mashambulio ya makombora ya wanamapambano wa Palestina.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *