Utafiti umebaini kuwa watoto 8 kati ya 10 wa shule nchini Afrika Kusini wanatatizika kusoma kufikia umri wa miaka kumi.
Afrika Kusini iliorodheshwa ya mwisho kati ya nchi 57 zilizofanyiwa tathmini katika Utafiti wa Kimataifa wa Kusoma na Kuandika, ambao ulijaribu uwezo wa kusoma wa wanafunzi 400,000 duniani kote mwaka wa 2021.
Kiwango cha kutojua kusoma na kuandika miongoni mwa watoto wa Afrika Kusini kilipanda kutoka asilimia 78 mwaka 2016 hadi 81.
Waziri wa Elimu nchini humo amehusisha matokeo hayo na kufungwa shule wakati wa janga la Covid-19.
Akielezea matokeo hayo kuwa “ya chini na ya kukatisha tamaa”, Angie Motshekga pia amesema mfumo wa elimu nchini Afrik Kusini unakabiliwa na changamoto kubwa za kihistoria, ikiwa ni pamoja na umaskini, ukosefu wa usawa na miundombinu duni.
Utafiti ulionyesha kuwa asilimia 81 ya watoto wa Afrika Kusini hawakuweza kusoma kwa ufahamu katika lugha yoyote kati ya 11 rasmi nchini humo.
Ikiwa pamoja na Morocco na Misri, Afrika Kusini ilikuwa mojawapo ya nchi tatu za Afrika ambazo zilishiriki katika tathmini za kufuatilia mienendo ya kusoma na kuandika na ufahamu wa kusoma wa watoto wa miaka tisa na 10.
Singapore ilishika nafasi ya kwanza katika viwango hivyo ikiwa na wastani wa alama 587, huku Afrika Kusini ikishika nafasi ya mwisho kwa pointi 288, chini ya Misri iliyokuwa na alama 378.
Utafiti pia ulionyesha kuwa kwa ujumla, wasichana walikuwa mbele ya wavulana katika ufahamu wao wa kusoma katika karibu nchi zote zilizotathminiwa; hata hivyo pengo la kijinsia limepungua katika duru ya hivi karibuni ya majaribio.