Watoto wa Kiyemeni wakusanyika mbele ya ofisi ya UN kupinga mauaji dhidi yao

Sambamba na maadhimisho ya Siku ya Watoto Duniani, watoto wa Kiyemeni wamekuanyika mbele ya ofisi ya Umoja wa Mataifa huko Sana’a mji mkuu wa nchi hiyo wakipinga mauaji yanayoendelea kufanywa na Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya watoto wa Yemen na kuzingirwa nchi yao.

Watoto wa Yemen leo Jumanne wameandamana katika mitaa mbalimbali ya mji wa Sana’a kwa lengo la kudhihirisha upinzani wao wa mashambulizi ya muungano vamizi wa Saudia na waitifaki wake. Watoto hao wameandama kupaza sauti zao ili jamii ya kimataifa ichukue hatua za kuwanusuru watoto ambao ndio wahanga wakuu wa hujuma na mashambulizi ya kila uchao ambayo yamevuruga maisha ya watoto na kuwafanya mayatima,  kuharibu ndoto zao na kuwanyima haki za kimsingi kabisa.

Afrah al-Khattabi, Afisa wa Mahusiano ya Umma wa mpango wa “Ndoto Yangu Ndogo” ameeleza kuwa, hii leo watoto wa Yemen wamekusanyika mkabala wa makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Sana’a ili kupaza sauti zao kwa walimwengu kuhusu namna haki zao zinavyokiukwa. Ameongeza kuwa wanataka sauti yao hiyo ifike duniani kote.

Binti mmoja wa Yemen aliyeshiriki kwenye maandamano hayo amesema kuwa: “Tumekusanyika hapa ili kufikisha ujumbe wetu kwa walimwengu wote kwamba tunataka kuishi kwa amani sawa kabisa na watoto wengine katika maeneo mbalimbali duniani. Tuna ndoto njema na hatutaki kuamshwa kwa milio ya makombora na risasi.”

Zaidi ya watoto milioni mbili wa Yemen hawaendi shule huku mateso yao ya kimwili na kiakili, ambayo yanaathiri moja kwa moja maisha yao, yakiongezeka kila siku.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *