Watu 10 wauawa Mogadishu katika shambulio la magaidi wa al-Shabab

Kwa akkali watu 10 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu kufuatia hujuma na mashambulio ya wanamgambo wa kundi la kigaidi la al-Shabab.

Maafisa wa usalama wanasema kuwa, watu hao 10 wameuawa baada ya wanamgambo wa al-Shabab kuvamia hoteli moja katika mji mkuu Mogadishu. Vyombo vya uusaama vinasema washambuliaji walilipua vilipuzi viwili nje ya hoteli hiyo kabla ya kuingia ndani ya jengo hilo na kufyatua risasi.

Wanaripotiwa kujifungia kwenye ghorofa ya juu ya Hoteli ya Hayat, saa chache baada ya mashambulizi kuanza.

Kitengo maalumu cha polisi kinasemekana kuwaokoa makumi ya wageni na wafanykazi kutoka hoteli hiyo.

Vikosi vya usalama viliendelea kuwadhibiti magaidi ambao wamezingirwa ndani ya chumba katika jengo la hoteli. Wengi wa watu waliokolewa, lakini takriban raia kumi walithibitishwa kufariki kufikia sasa,” alisema afisa mmoja, Mohamed Abdikadir.

Magari mawili ya mabomu yalilenga Hotel ya Hayat,” afisa wa polisi aliambia shirika la habari la Reuters katika taarifa. “Moja liligonga kizuizi karibu na hoteli, na kisha jingine  likakagonga lango la hoteli. Tunaamini wapiganaji wako ndani ya hoteli.”

Tangu mwaka 1992, Somalia haijawahi kuwa na utulivu wa japo siku moja kutokana na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe na mashambulizi ya genge la kigaidi la al Shabab.

Genge hilo lilianzishwa mwaka 2004 na lenyewe limejitangaza kuwa ni sehemu ya mtandao wa kigaidi wa al Qaida.

Genge hilo mara kwa mara limekuwa likishambulia wanajeshi wa serikali na askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika hasa katika mji mkuu Mogadishu na pia huwa linafanya mashambulizi ya mara kwa mara ya raia wa Somalia.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *