Watu wasiopungua 180 wamefariki dunia nchini Afghanistan kutokana na mafuriko na matukio yanayohusiana na mvua kali zilizonyesha hivi karibuni.
Msemaji wa serikali ya Taliban nchini humo, Zabihullah Mujahid amesema mbali na watu 182 kuaga dunia kwenye janga hilo la kimaumbile, wengine zaidi ya 250 wamejeruhiwa.
Amesema nyumba zaidi ya 3,000 zimesombwa na maji ya mafuriko hayo na kusababisha maelfu ya familia kuachwa bila makazi, huku maelfu ya mifugo ikighariki kwenye janga hilo.
Msemaji wa Taliban ametoa mwito kwa mashirika ya kimataifa na nchi za Kiislamu kuisaidia Afghanistan, ambayo kwa sasa inakabiliwa na mgogoro wa kibinadamu kutokana na majanga hayo.
Mwaka uliopita pia, mamia ya watu walifariki na kujeruhiwa na nyumba nyingi zilibomoka kutokana na mafuriko na maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kali za msimu zilizonyesha katika maeneo mbalimbali ya Afghanistan.
Tangu Taliban ichukue udhibiti wa Afghanistan mwaka mmoja uliopita, nchi hiyo imeshuhudia majanga kadhaa ya kimaumbile ukiwemo ukame na mtetemeko wa ardhi ulioa watu zaidi ya 1,000 mwezi Juni mwaka huu.