Watu 20 wauawa Somalia katika shambulio la kigaidi la al-Shabab

Watu wasiopungua 20 wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa kufuatia shambulio la kigaidi la al-Shabab katikati mwa Somalia.

Duru za usalama zinasema kuwa, shambulio hilo la al-Shabab lililolenga mabasi kadhaa katika mji wa Hiran katikati mwa Somalia limetokea Jumamosi ya leo na kwamba, wanawake na watoto ni miongoni mwa waliouawa katika shambulio hilo.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, mabasi kadhaa ya abiria yameungua moto baada ya milipuko hiyo kwenye mji wa Beledweyne.

Shambulio la leo ni mlolongo wa mashambulio ya kigaidi ya kundi la wanamgambo wa al-Shabab nchini Somalia ambao wamehatarisha usalama na maisha ya wananchii wa nchi hiyo.

Tangu mwaka 1992, Somalia haijawahi kuwa na utulivu wa japo siku moja kutokana na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe na mashambulizi ya genge la kigaidi la al Shabab.

Genge hilo lilianzishwa mwaka 2004 na limejitangaza kuwa ni sehemu ya mtandao wa kigaidi wa al Qaida.

Mara kwa mara kundi la kigaidi la al-Shabab limekuwa likishambulia wanajeshi wa serikali na askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika (AMISOM) hasa katika mji mkuu Mogadishu, kama ambavyo limekuwa likiwashambulia mara kwa mara raia wa Somalia katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *