Watu zaidi ya 30 wauawa katika shambulio la kigaidi katikati ya Mali

Watu wasiopungua 31 wameuawa katikati ya Mali huko magharibi mwa Afrika baada ya wanamgambo waliokuwa na silaha kushambulia basi iliyokuwa imebebe raia wa kawaida wakielekea sokoni. Watu wenye silaha wasiofahamika walianza kufyatua risasi na kisha kumuuwa dereva kabla ya kulichoma moto basi hilo.

Faraan: Shirika la habari la EFE limeripoti kuwa, akthari ya waliouliwa ni wanawake ambao walikuwa wakielekea sokoni sehemu yao ya kazi. Shambulio hilo la kigaidi dhidi ya basi la abiria limetajwa kuwa kubwa zaidi kuwahi kuikumba nchi ya Mali katika siku za hivi karibuni.

Moulaye Guindo Meya wa mji wa Bankass ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa watu waliokuwa na silaha walianza kulipiga risasi basi la abiria, kukata matairi na kisha kuwapiga risasi abiria. Ameongeza kuwa abiria wengine waliokuwa katika basi hilo hadi sasa hawajulikani walipo.

Weledi wa mambo wanasema kuwa, basi hilo la abiria liliviziwa na magaidi hao wenye silaha kwa kuzingatia kuwa hufanya safari mara mbili kwa wiki kutoka katika kijiji cha Songo hadi katika soko la Bandiagara, safari yenye umbali wa kilomita 10.

Shambulio hilo la kikatili limetekelezwa katika mkoa wa Mopti katikati ya Mali; eneo ambalo mara kwa mara linathiriwa na machafuko na mashambulizi ya magaidi wa mtandao wa al Qaida na kundi la Daesh.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *