Wauguzi wapatao laki moja kote nchini Uingereza wameanza mgomo kushinikiza malipo bora na mazingira mazuri ya kazi.
Wauguzi hao wanafanya mgomo kushinikiza nyongeza ya mshahara kwa asilimia 19, ingawaje serikali ya London imekuwa ikisisitiza kuwa inaweza tu kuwapa nyongeza ya asilimia 4 hadi 5.
Waziri wa Afya wa Uingereza, Steve Barclay amesema, “Inasikitisha kuona wanachama wa muungano wa wauguzi wametekeleza kweli kivitendo vitisho vya kufanya mgomo.”
Wauguzi nchini Uingereza, Wales na Ireland Kaskazini walifanya mgomo jana Alkhamisi, baada ya chama chao cha Royal College Nursing ( RCN) kusema kwamba, serikali imekataa kusikiliza malalamiko yao.
Mgomo huu ni wa kwanza katika historia ya miaka 106 ya chama hicho cha wauguzi, na unatazamiwa kufanyika tena Disemba 20 kwa ajili ya kushinikiza malipo bora.
Mgomo huo umeathiri pakubwa sekta ya afya nchini Uingereza, huku miito mbalimbali ikitokela kuitaka serikali ya London kuitisha kikao cha mazungumzo na wauguzi hao; na pande mbili hizo kufikia mwafaka.
Wauguzi hao wamesema serikali haina budi kuwaongeza mishahara kwa asilimia 19, kutokana na mfumko wa bei ambao umepanda kwa karibu asilimia 12, ongezeko ambao halijawahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 41 iliyopita nchini Uingereza, na kupelekea kuongezeka kwa bei za chakula na nishati.