Wavuvi 14 Wairani waliokuwa wanashikiliwa mateka na wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabaab nchini Somalia wamewasili nchini Iran baada ya kuachiwa huru.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetangaza habari hiyo na kueleza kuwa, mabaharia hao waliokuwa wametekwa nyara na wanamgambo wa al-Shabaab miaka minane iliyopita wameachiwa huru kutokana na jitihada za kidiplomasia za wizara hiyo.
Taarifa ya wizara hiyo imeeleza kuwa, mabahari hao wa Kiirani waliotekwa nyara na al-Shabaab katika maji ya kimataifa mwaka 2015, waliwasili jana usiku katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Imam Khomeini hapa Tehran wakitokea Mogadishu, mji mkuu wa Somalia.
Agosti mwaka 2020, kundi jingine la mabaharia Wairani ambao walikuwa wametekwa nyara na maharamia wa Somalia mwaka 2015 waliachiliwa huru na kurejea nchini.
Kabla ya hapo pia, makundi mengine mawili ya mateka raia wa Iran waliachiliwa huru na kurejea nyumbani kutokana na jitihada za idara kadhaa za Iran zikishirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu.
Katika hatua nyingine, jeshi la Somalia limetangaza habari ya kuangamiza mamia ya wanachama wa kundi la wapiganaji wa al-Shabaab katika eneo la Shabelle ya Kati.
Jenerali Mohamed Tahlil, Kamanda wa Kikosi cha Nchi Kavu cha Jeshi la Somalia amesema askari wa nchi hiyo wameshambulia maficho ya magaidi hao katika kijiji cha El-Ba’ad eneo la Shabelle ya Kati, na kuua magaidi 67, na hivyo kupelekea idadi ya wanachama wa al-Shabaab waliouawa katika eneo hilo ndani ya wiki moja kupindukia 210.