Jana Ijumaa, wananchi wa Yemen walifanya maandamano makubwa katika mikoa mbalimbali kulaani uvamizi wa muungano wa Saudia na Marekani dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu na kuendelea kuzingirwa kila upande nchi yao pamoja na vitendo mbalimbali vya kuchochea vita vinavyofanya na madola vamizi.
Kwa mujibu wa televisheni ya al Alam, mamia ya maelfu ya wananchi wa Yemen wameshiriki kwenye maandamano hayo ya kitaifa yaliyofanyika jana mjini Saada na kwenye mikoa mingine kulaani kuendelea kuzingirwa Yemen, hujuma za kila namna na mashambulio ya kijeshi za muungano vamizi wa Saudia na Marekani dhidi ya nchi hiyo.
Kamati iliyoandaa maandamano hayo ilikuwa imewataka watu kujitokeza kwa maelfu barabarani ili kufanikisisha maandamano hayo. Kamati hiyo iliwaomba pia watu wa Sana’a, mji mkuu wa Yemen, na miji mingine ya nchi hiyo nao kushiriki kwa wingi ili kuwaonesha walimwengu kuwa taifa la Yemen liko hai na liko pamoja na jeshi na kamati za kujitolea za wananchi wa nchi hiiyo.
Kamati hiyo pia iliwataka wananchi kulaani uvamizi na kukendelea kuzingirwa Yemen kunaofanywa na muungano vamizi wa Saudi Arabia, Marekani na Imarati na kusumama kidete kukabiliana na uchokozi huo.
Kwa upande wake televisheni ya Al-Masirah imeripoti kwamba maandamano ya jana ya watu wa Yemen yamefanyika Saada kwa kauli mbiu “kuzingirwa ni vita.” Washiriki wa maandamano hayo wamebeba pia picha za Abdul Malik al-Houthi, kiongozi wa harakati ya Ansarullah, na kulaani sera za kibeberu na za kupenda vita za Marekani.
Maandamano mengine kama haya yalifanyika pia jana katika mikoa ya Sana’a, Taiz, Ibb, Dhamar, al Hudaydah, Al Bayda, Hajjah, Imran, Al Jouf na Ma’rib