Wayemen walivyojiimarisha kwa nguvu za kijeshi kuzuia adui asijusuru kuanzisha mashambulio

Wakati mwaka wa nane wa vita vilivyoanzishwa na muungano wa kijeshi wa Saudi Arabia dhidi ya Yemen ukiwa unaendelea kupita, Wayemen wanazidi kuongeza nguvu na uwezo wao wa kijeshi wa kumzuia adui asithubutu kuanzisha mashambulio dhidi ya nchi hiyo.

Mwaka wa nane wa vita ulivyoanzisha muungano wa Saudia dhidi ya Yemen umeambatana na kuanza usitishaji vita uliopendekezwa na Umoja wa Mataifa. Miezi mitano ya usitishaji vita huo imepita huku Wayemeni wakiitumia fursa hiyo kuonyesha nguvu na uwezo wao wa kijeshi. Gwaride na mazoezi maalumu ya kijeshi ya kuonyesha uwezo wa makombora wa vikosi vya jeshi la Yemen vilifanyika hivi karibuni katika bandari ya Al Hudaydah magharibi mwa nchi, ambapo jeshi na harakati ya Ansarullah zilionyesha sehemu ya nguvu na uwezo wao katika medani za vita. Hayo yalikuwa mazoezi makubwa zaidi ya kijeshi kufanywa na vikosi vya Yemen, yaliyojumuisha silaha na zana mpya kabisa za kivita za nchi kavu, angani na baharini.

Mazoezi hayo ya kijeshi yalikuwa na salamu na jumbe muhimu kadhaa za kufikisha:

Ujumbe wa kwanza ni kwamba, Wayemen wana irada na azma thabiti ya kukabiliana na muungano vamizi wa Saudia na kulinda ardhi zao zote pamoja na mamlaka ya nchi yao; na vita vya miaka minane havijawavunja moyo wala kuwakatisha tamaa ya kupata ushindi na kufikia malengo yao. Na ijapokuwa Wayemen hawataki vita hivyo viendelee, lakini kuendelea kwake hakuwatii hofu na wako tayari kulinda ardhi zao zote, na hili ndilo lengo lao kuu katika vita hivyo visivyo na mlingano kati yao na Wasaudia.
Ujumbe mwingine muhimu wa mazoezi hayo ya kijeshi ni kwamba, Wayemen hawajasita wala kuzembea hata kidogo kuimarisha nguvu zao za kumbana adui asithubutu kushambulia; na hali yao ya kijeshi hii leo haiwezi kulinganishwa na miaka minane iliyopita. Kuhusiana na suala hilo, Yasser Al-Houri, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amesisitiza katika mahojiano na shirika la habari la IranPress kwamba, Yemen imewatumia jumbe na salamu kadhaa wavamizi kupitia mazoezi hayo ya kijeshi; muhimu zaidi ni kwamba, baada ya miaka minane, jeshi la Yemem haliko tena katika hali yake ya zamani, bali lina nyenzo na uwezo mkubwa wa kumsababishia adui madhara na hasara kubwa.

Ujumbe mwingine muhimu wa maneva hayo ni kwamba, ikiwa adui Saudia ataendelea kukiuka usitishaji vita na kuandaa mazingira ya kuvunjika makubaliano ya kusitisha mapigano, ajue kwamba Wayemen wamejiandaa ipasavyo kutoa vipigo vikali kwa muungano vamizi unaoongozwa na utawala huo wa Riyadh. Kwa maneno mengine ni kuwa, kurefuka vita sio lengo la Wayemen, lakini wameshajiweka tayari kwa vita vya muda mrefu. Kwa hakika tunaweza kusema, mazoezi hayo ya kijeshi ni aina fulani ya indhari kwa muungano wa Saudia kuutaka ujihadhari na kuvuruga makubaliano ya usitishaji vita.

Salamu nyingine muhimu za maneva hayo ni kwamba, Wayemen wamefikia hitimisho kuwa kimsingi, hakuna matumaini yoyote kwa mfumo unaotawala dunia kwamba utachukua hatua ya kusimamisha mashambulio ya Saudia; hivyo njia pekee ya kukomesha vita ni kutegemea uwezo wao wenyewe na kuimarisha nguvu na uwezo wa kumfanya adui wa Kisaudi asifikirie kuanzisha mashambulio.
Ukweli wa mambo ni kwamba, kilichoulazimisha muungano wa Saudia ukubali usitishaji vita ni kuimarishwa nguvu na uwezo wa Wayemen wa kuzuia hujuma katika kipindi chote cha vita. Katika miaka ya karibuni, Wayemen wametoa vipigo vikali hasa kwa Saudi Arabia, ikiwemo kushambulia vituo vya mafuta vya shirika la Aramco, operesheni ambazo zilitekelezwa mara kadhaa. Kuimarishwa nguvu za Yemen za uzuiaji hujuma kumewatia hofu Wasaudia na vilevile kumechafua itibari yao ya kisiasa na kijeshi mbele ya walimwengu, kwa sababu mtoaji vipigo hivyo ni nchi dhaifu na maskini zaidi ya Kiarabu katika eneo.
Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *