Gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth limeashiria matatizo makubwa yanayowakumba waandishi wa habari wa utawala wa Kizayuni katika mashindano ya Kombe la Dunia 2022 yanayoendelea hivi sasa nchini Qatar na kuandika, katika mashindano haya tumeelewa ni kiasi gani hatupendwi na tunachukiza vibaya katika ulimwengu wa Kiarabu.
Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, gazeti hilo la Kizayuni limeandika katika ripoti yake kuwa, waandishi wa habari wa utawala wa Kizayuni wa Israel waliotumwa Qatar kuakisi mashindano ya Kombe la Dunia ya Kandanda 2022 wanakabiliwa na wakati mgumu.
Waaandishi wa utawala wa Kizayuni wamesusiwa kikamilifu na wanashindwa kufanya mahojiano na watu, kwani kila wanapojitambulisha kuwa ni kutoka Israel, Waarabu wanawakwepa kama ukoma huku wengine wakisema waziwazi kuwa katika dunia hakuna kitu kinachoitwa Israel.
Tovuti ya televisheni ya Al Mayadeen nayo imelinukuuu gazeti la hilo la Kizayuni la Yedioth Ahronoth likisema: “Tumeelewa vizuri ni kiasi gani Israel haipendwi katika ulimwengu wa Kiarabu.”
Limeendelea kuandika: “Chuki hiyo si ndani ya tawala na wakuu wa nchi tu, bali hata mitaani na kati ya watu wa kawaida, kila unayemuangalia unamuona anaichukia vibaya Israel.”
Gazeti hilo la Kizayuni limemnukuu mwandishi wake mmoja akisema: “Baada ya kupitisha siku 10 nikiwa Doha (mji mkuu wa Qatar), nimeshindwa kuelewa tumekumbwa na nini hapa. Tunapenda kusema ukweli wa mambo. Tunahisi kuwa watu wote hapa wanatuchukia.”
Siku chache zilizopita pia, mwandishi mmoja Mzayuni, Ben Hamo, ambaye anaelewa vizuri lugha ya Kiarabu na ni Mzayuni mwenye chuki ambaye anajigamba waziwazi kuwa yeye ni Mzayuni, alisema waziwazi kuwa, tusijidanganye, Waarabu hawaupendi kabisa utawala wa Kizayuni.