Duru moja ya Kizayuni imethibitisha taarifa kuwa jeshi la Israel lina kiwewe cha kuingia vitani tena na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon na kusisitiza kuwa, utawala huo unavichukulia kwa uzito mkubwa vitisho vya Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sayyid Hassan Nasrullah.
Mtandao wa habari wa News1 wa Kizayuni umeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, utawala wa Kizayuni umeitumia ujumbe serikali ya Lebanon kupitia mpatanishi Mmarekani, Amos Hochstein ikitaka kupewa dhamana kwamba Hizbullah haitatoa vitisho vyovyote vya kushambulia visima vya gesi katika Bahari ya Mediterranean hadi yatakapomalizika mazungumzo ya kuchorwa mipaka baina ya pande hizo mbili, katikati ya mwezi ujao wa Septemba.
Ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel, zina mzozo wa mpaka na Lebanon katika Bahari ya Mediterranean. Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon imeuonya utawala wa Kizayuni kwamba usitumie ujanja wake wa kila siku wa kupoteza wakati bali muda uliopangwa ukimalizika yaani katikati ya mwezi ujao wa Septemba, Hizbullah haitojifunga tena na machakato wa mazungumzo hayo.
Afisa huyo wa utawala wa Kizayuni ameiambia tovuti ya News1 kwamba Hizbullah hata hivi sasa haitaki kufungamana na mchakato wa mazungumzo na inaamini kuwa Lebanon ndiyo yenye haki za kuvuna gesi katika eneo linalozozanishwa la Bahari ya Mediterranean, hivyo serikali ya Lebanon inapaswa kutoa dhamana kwa Israel.
Mazungumzo ya kuchorwa mipaka baina ya Lebanon na utawala wa Kizayuni yalianza mwezi Oktoba 2020 kwa kusimamiwa na Umoja wa Mataifa na kwa upatanishi wa Marekani. Lakini ni kawaida ya utawala wa Kizayuni kutoheshimu ahadi zake na kupoteza wakati. Hivyo Hizbullah ya Lebanon imesema, haiwezi kusubiri muda wote kupotezewa wakati na utawala huo pandikizi.