Arusha. Wenyeviti wa Bodi za Maji nchini wametakiwa kudhibiti na kuhakikisha wanasimamia mamlaka za maji ili wananchi wasibambikiwe ankara za maji ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na baadhi ya wananchi.
Agizo hilo limetolewa leo Juni 29, 2022 na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akifungua mafunzo ya siku tatu ya Bodi na Menejimenti za Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira nchini unaofanyika jijini hapa.
Amesema bodi hizo zinapaswa kudhibiti ankara za maji ili zinazowafikia wateja ziwe zilizoidhinishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji(Ewura).
Amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakibambikiwa ankara za maji jambo ambalo limekuwa likisababisha malalamiko hivyo wenyeviti hao wanapaswa kusimamia na kudhibiti suala hilo.
“Simamieni mamlaka za maji, bili ziwe zimeidhinishwa na Ewura yaani ziwe bili halisia. Hatutasita kuvunja bodi ambazo bill zake zinazotolewa kwa wananchi zitakuwa hazijaidhinishwa na Ewura, tusimamie bili zisiwe bambikizi,” amesema.
Kuhusu kuunganishwa maji, amesema serikali inatumia fedha nyingi kuhakikisha wananchi wanapata majisafi na salama kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa nchini, lakini baadhi ya maeneo wananchi wakiomba kuunganishiwa maji inachukua muda mrefu huku jambo hilo likisababisha kuonekana kwa dalili ya rushwa.
Aidha amezitaka bodi hizo kuwa na mshikamano ili waweze kufanya kazi kwa pamoja na pale panapohitajika maamuzi waweze kutoa kwa wakati.
“Bodi isipokuwa na umoja na mshikamano hamtaweza kufanya maamuzi,zipo bodi Mwenyekiti anaongea hili wajumbe wanaongea lao,hili siyo sawa. Mfano Arusha, Bukoba, Lindi mnafanya kazi nzuri hata Dodoma licha ya changamoto ya maji mnafanya vizuri,” amesema Waziri huyo.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Anthony Sanga amezitaka bodi hizo kuweka taratibu za kuwa na vikao na watumishi wake ili kubaini changamoto na kuzitatua kwa wakati.
“Wizara inapitia mapinduzi makubwa kwani imekuwa wizara ya utatuzi wa changamoto za maji na kuondoka kwenye wizara ya malalamiko,” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira kutoka Wizara hiyo, Joyce Msiru amesema mafunzo hayo, yameshirikisha washiriki 145 ambapo kwa muda wa siku hizo tatu mada 12 zitawasilishwa na wajumbe hao kuzijadili kwa pamoja.