Wizara ya Intelijensia ya Iran imetekeleza oparesheni kadhaa zilizofanikiwa dhidi ya utawala wa Israel katika miezi ya hivi karibuni sambamba na kuzima idadi kubwa ya njama za utawala huo wa Tel Aviv na waitifaki wake magaidi dhidi ya Iran.
Waziri wa Intelijensia Esmail Khatib ameyasema hayo Jumatano mjini Tehran katika mkutano na Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) Mohammad Baqer Qalibaf.
Khatib amesema oparesheni hizo zinaashiria uwezo wa kiusalama wa Wizara ya Intelijensia ya Iran. Ameongeza kuwa, maadui wamefeli katika njama zao za kuvuruga usalama wa Iran na kubaini kuwa moja ya sababu za kugonga mwamba njama hizo ni ushirikiano wa wananchi na wizara ya intelijensia na pia azma ya serikali ya sasa ya kuhakikisha kuna usalama endelevu nchini.
Aidha amesema wizara yake ina wajibu wa kupambana na ugaidi, utawala wa Kizayuni na njama za uharibifu nchini.
Mapema wiki hii Wizara ya Intelijensia ya Iran ilitangaza habari ya kutiwa mbaroni majasusi kadhaa waliokuwa wakitumikia shirika la ujasusi la Israel (Mossad). Taarifa ya wizara hiyo imeeleza kuwa, vyombo vya usalama vya Jamhuri ya Kiislamu vimewatia nguvuni majasusi hao waliojipenyeza nchini kupitia eneo la Kurdistan, magharibi mwa Iran. Kwa mujibu wa Wizara ya Intelijensia ya Iran, maajenti hao wa utawala wa Kizayuni wa Israel walikuwa wametumwa hapa nchini kufanya mashambulizi ya kigaidi, sambamba na kuvamia maeneo nyeti ya taifa hili.
Taarifa ya wizara hiyo imeeleza kuwa, majasusi hao wa utawala haramu wa Israel walikuwa na suhula na vyombo vya kisasa kabisa vya mawasiliano na mada za miripuko. Iran imefanikiwa kutwaa silaha hizo za maadui.