Waziri Mkuu wa Burkina Faso, Apollinaire Kyelem de Tambela amesema, Ukraine inayasaidia makundi ya magaidi katika eneo la Sahel barani Afrika; na inafanya hivyo kwa nia ya kuidhoofisha Russia ambayo inashirikiana kijeshi na nchi za eneo hilo.
Tambela ambaye yuko nchini Russia anakohudhuria kongamano la Siku za Kiuchumi za Burkina Faso, ameeleza hayo katika mahojiano na Russia Today, wakati akijadili njia za kukabiliana na ugaidi nchini Mali, ambayo ni jirani wa kaskazini wa nchi yake.
“Kwa nini Waukraine walianza kusaidia magaidi katika eneo letu? Ni kutaka kuiumiza Russia, kwa sababu wanajua kwamba Warussia wana ushirikiano wa kijeshi katika suala la usalama na nchi tatu. Na kwa hivyo, Ukraine inataka kuidhoofisha Russia ili kuwa na udhibiti wa nchi zetu tatu”, ameeleza mkuu huyo wa chombo cha diplomasia cha Burkina Faso.
Akieleza athari kubwa na hasi za hatua hiyo ya serikali ya Kiev, Tambela amesema: “kujaribu kuidhoofisha Russia, kutakuwa na athari kwa maadui zetu, ambao ni magaidi, kwa hivyo hatuwezi kukubali hilo … Wale wanaoshambulia Mali wanaishambulia pia Burkina Faso”; na akaongezea kwa kusema: “Ukraine inapaswa itatue matatizo yake yenyewe ndani ya nchi yake”.
Mwezi Agosti, serikali ya kijeshi ya Burkina Faso iliungana na Mali na Niger kulitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lichukue hatua dhidi ya Ukraine kwa madai ya kuwapa waasi taarifa za kijasusi kufanikisha shambulio la kuvizia ambalo liliua makumi ya wanajeshi wa Mali na wapiganaji wa kundi Wagner.
Bamako na Niamey zimevunja uhusiano wa kidiplomasia na Kiev kulalamikia hatua hiyo, licha ya serikali ya Ukraine kukanusha madai hayo kufuatia msukosuko huo.