Waziri Mkuu wa Italia akosoa sera za ukoloni na unafiki wa Ufaransa kuhusu wahamiaji

Waziri Mkuu wa Italia ameikosoa hadharani Ufaransa kwa mtazamo wake wa kinafiki kuhusu suala la wahamiaji wanaotoka Afrika, ambalo limekuwa mzozo kati ya nchi hizo mbili katika wiki za karibuni huku akifichua sera ya ukoloni ya Paris huko Burkina Faso.

Giorgia Meloni, ambaye alikuwa akizungumza katika mahojiano ya televisheni, ameyasema hayo huku akionyesha picha ya mtoto anayefanya kazi katika machimbo ya dhahabu nchini Burkina Faso, ambayo ni moja ya nchi maskini zaidi duniani.

Amesema Ufaransa ingali inachapisha fedha za dhahabu za kikoloni kwa ajili ya nchi hiyo na “inashurutisha kwamba asilimia 50 ya kila kitu ambacho Burkina Faso inauza nje kiishie kwenye mfuko wa hazina ya Ufaransa.”

Waziri mkuu wa Italia ameendelea kusema kuwa, “Dhahabu ambayo mtoto huyu huteremka kwenye handaki kuchimba, mara nyingi huishia kwenye hazina ya jimbo la Ufaransa.”

Meloni ameongeza, “Kwa hiyo, suluhisho [la suala la wahamiaji] sio kuwachukua Waafrika na kuwaleta Ulaya. Suluhisho ni kuikomboa Afrika kutoka kwa Wazungu fulani wanaoitumia vibaya na kuwaruhusu watu hawa kuishi katika umasikini.”

Matamshi ya Meloni yamekuja wakati Ufaransa imekuwa ikiendeleza mashambulizi ya maneno dhidi ya Italia baada ya maafisa wa Rome kuamua kuwazuia wahamiaji waliokuwa kwenye meli iitwayo Ocean Viking kuteremka katika ardhi ya nchi hiyo.

Kufuatia uamuzi huo Ufaransa imesema itairuhusu meli hiyo iliyokuwa ikisafirisha zaidi ya wakimbizi 200 kutia nanga katika pwani yake ya kusini huku Waziri wa Mambo ya Ndani  wa nchi hiyo Gerald Darmanin akisema meli hiyo ya Ocean Viking ambayo abiria wake ni watoto 57 itaruhusiwa kutia nanga katika bandari ya kijeshi ya Toulon.

Darmanin amesema marufuku ya serikali ya Italia ya mrengo wa kulia kwa meli hiyo, ambayo ilikuwa imekwama kwa siku kadhaa karibu na Sicily, ilikuwa “ya kulaumiwa” na “ya ubinafsi.” Darmanin ameutaja  msimamo wa Italia kuwa “usioeleweka.”

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *