Waziri Mkuu wa Mali alalamika dhidi ya uungaji mkono wa Ufaransa kwa magenge ya kigaidi

Waziri Mkuu wa Mali, Choguel Kokalla Maiga, ameishutumu serikali ya kikoloni ya Ufaransa kwa vitendo vyake vilivyo dhidi ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika na kusema kuwa, Wafaransa walipaswa kutusaidia, lakini badala yake wanayasaidia magenge ya kigaidi yanayopigania kujitenga na wanazichochea nchi za Ulaya ziiwekee vikwazo nchi ya Mali.

Ameishutumu vikali Ufaransa kwa kutoheshimu makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi yaliyofikiwa baina yao na kusisitiza kuwa, ilivyopaswa kufanya Paris ni kuisaidia serikali ya Mali kupambana na magaidi lakini mkoloni huyo kizee wa Ulaya anafanya kinyume chake kabisa, anayasaidia makundi ya kigaidi na kuigawa vipande vipande nchini hiyo. Mwaka wa 9 wa ahadi za Paris za kupambana na ugaidi nchini Mali umekaribia kumalizika, lakini si tu mgogoro wa ugaidi haujaisha nchini humo, bali umeenea zaidi. Wakati Ufaransa ilipotoa ahadi za kulisaidia taifa la Mali kupambana na ugaidi, vitendo vya kigaidi vilikuweko kwenye maeneo ya kaskazini mwa Mali tu, lakini hivi sasa ugaidi umeenea katika asilimia 80 ya ardhi ya nchi hiyo. Waziri Mkuu wa Mali amesema, Ufaransa inataka kuifanya nchi yetu kuwa muhanga wa vita vya jeopolitiki na istratijiki baina ya Russia na Magharibi.

Baada ya kutokea mapinduzi ya kwanza ya kijeshi mwaka 2012 huko Mali na baadaye kuzuka machafuko nchini humo, magenge kadhaa ya kigaidi ambayo yalijitangaza kuwa na mfungamano na mitandao ya al Qaida na Daesh (ISIS) yalianzisha uasi kaskazini mwa Mali. Mkoloni Ufaransa alitumia kisingizio hicho kumimina wanajeshi wake nchini Mali kwa madai ya kupambana na magenge hayo ya kigaidi. Serikali ya Mali ilikubali kushirikiana na Ufaransa kupambana na magaidi lakini ilichotaka serikali ya Bamako ni msaada wa taarifa tu za kijasusi na mashambulizi ya anga, kutoka kwa Ufaransa. Serikali ya Mali haikuzungumzia kabisa suala la kutumwa wanajeshi wa Ufaransa nchini humo. Ijapokuwa katika baadhi ya maeneo, Ufaransa imetekeleza mapatano yake na serikali ya Bamako, lakini pia wakoloni hao wa Ulaya walizuia jeshi la Mali kuingia katika mji wa Kidal wa kaskazini mwa nchi hiyo na badala yake waliukabidhi mji huo kwa kundi liitwalo Ansaruddin ambalo limejitangaza kuwa ni tawi la mtandao wa kigaidi wa al Qaida nchini Mali. Hatua hiyo ya mkoloni Ufaransa, iliikasirisha mno serikali ya Mali.

Waziri Mkuu wa Mali anasema, serikali ya nchi hiyo haiwezi kuingia katika mji wa Kidal na eneo hilo lote hivi sasa linadhibitiwa na Ufaransa na magenge yenye silaha ambayo yanapewa mafunzo ya kijeshi na maafisa wa Ufaransa. Amesema, wana ushahidi kamili na madhubuti wa kuthibitisha jambo hilo.

Baada ya kikao cha mwezi Julai 2021 kilichofanyika kwa njia ya Intaneti na kushirikisha kundi la nchi za Sahel Afrika ikiwemo Mali, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alitangaza kuwa Paris inafuatilia suala la kupunguza idadi ya wanajeshi wake kwenye eneo hilo. Alisisitiza kuwa, ifikiapo katikati ya mwaka 2021 kambi za kijeshi za Ufaransa za kaskazini mwa Mali zitafungwa na wanajeshi wa nchi hiyo watapelekwa kusini mwa Mali. Wakati yalipotamkwa maneno hayo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Mali ilimwita balozi wa Ufaransa mjini Bamako na kumkabidhi malalamiko ya nchi hiyo kutokana na matamshi yasiyo na urafiki ya Emmanuel Macron.

Ijapokuwa Macron alidai wanajeshi wa Ufaransa wataondolewa katika kambi za kijeshi za kaskazini mwa Mali, lakini wakati huo huo alisema, Paris itaendele kuwa na wanajeshi baina ya 2500 na 3000 kutoka 5000 waliokuweko wakati huo kwenye eneo la Sahel Afrika. Alidai wanajeshi hao watakaobakia, kazi yao itakuwa ni kutoa mafunzo ya kijeshi kwa askari wa nchi za eneo hilo.

Abdul Wahid Oulad Mouloud, mtaalamu wa masuala ya kiusalama anasema, kitendo cha Paris cha kung’ang’ania kubakia wanajeshi wake katika nchi ya Mali ni jambo lililotarajiwa kabisa. Hii ni kwa sababu Ufaransa ni mkoloni mkongwe na kizee wa Ulaya na eneo la Sahel Afrika linahesabiwa na Paris kuwa ni eneo la jadi kwa Ufaransa. Paris haiko tayari kabisa kuona inapoteza ushawishi wake kwenye eneo hilo hasa wakati huu ambapo kuna migogoro ya kimataifa na ushindani wa madola ya dunia huku kila mmoja akipigania kuwa na ushawishi zaidi kuliko mwingine

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *