Waziri Mkuu wa Sudan kutangaza kujiuzulu katika masaa machache yajayo

Duru za karibu na Waziri Mkuu wa Sudan Abdallah Hamdok zimetangaza kwamba waziri mkuu huyo atatangaza kujiuzulu katika kipindi cha masaa machache yajayo.

Faraan: Vyombo mbalimbali vya habari vimeripoti habari hiyo na kuzinukuu duru mbili zilizoko karibu na Hamdok zikisema kuwa, waziri mkuu huyo wa Sudan atatangaza kujizulu masaa machache yajayo.

Hamdok alirejea madarakani tarehe 21 mwezi uliopita wa Novemba baada ya mwezi mmoja kabla yake kupinduliwa na jeshi na kusambaratishwa serikali ya mpito iliyokuwa imeshirikisha raia na wanajeshi.

Majenerali wa kijeshi wakiongozwa na Abdul Fattah Burhan waliipindua serikali yake mwezi Oktoba mwaka huu na kuzusha hasira kubwa za wananchi ambao wanaendelea na maandamano hadi leo hii.

Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Novemba, Abdallah Hamdok alikubali kurejea madarakani akidai ni kwa ajili ya kuokoa roho za raia wanaokandamizwa na wanajeshi wa nchi hiyo. Hata hivyo hatua yake hiyo hata haikupunguza hasira za wananchi na kila leo maandamano yanaendelea ya kushinikiza wanajeshi warejee makambini na waruhusu serikali ya raia itawale nchini Sudan.

Shirika la habari la Reuters limetangaza kuwa waandamanaji 47 wameshauliwa na wanajeshi katika maandamano wakiwemo raia wawili waliouawa Jumamosi wiki hii. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, jana Jumanne pia Umoja wa Mataifa ulisema kwamba umepokea ripoti za wanawake na wasichana kunajisiwa na makundi ya watu huko Sudan.

Kabla ya hapo duru za karibu na Abdallah Hamdok zilisema kuwa, waziri mkuu huyo atabakia madarakani iwapo tu atapata uungaji mkono wa kisiasa na iwapo jeshi litaheshimu makubaliano yaliyofikiwa. Uamuzi wake wa kujiuzulu unaonesha masharti yote hayo hayakutekelezwa.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *