Waziri Mkuu wa Uingereza Liz Truss ajiuzulu

Waziri Mkuu wa Uingereza Liz Truss amejiuzulu wadhifa wake huo leo baada ya kuushikilia kwa siku 45 tu.

Katika hotuba fupi, Truss amesema inabidi kuondoka madarakani kwa ajili ya umoja wa chama chake cha Conservative na maslahi ya taifa.

Liz Trus amekuwa akikabiliwa na mashinikizo makubwa kutoka ndani ya chama cha kihadhina kufuatia sera ya kiuchumi ambayo imekosolewa sana.

Kujiuzulu kwake kumetokea muda mfupi baada ya kujiuzulu kwa Waziri wa Mambo ya Ndani Suella Braverman.

Hata hivyo Liz Truss atasalia kuwa Waziri Mkuu hadi chama cha conservative kitakapomteua kiongozi mwingine. Amesema kwamba wakati chama cha conservative kinamtafuta mrithi wake, ataendeela kutekeleza sera za kiuchumi kwa ajili ya taifa.

Mpango wake wa kupunguza bajeti ulitikisa soko la fedha na kupelekea chama chake cha kumshinkiza kuondoka madarakani.

Katika taarifa fupi, Truss amesema, “Tulikuwa na nia ya kuweka kiwango cha chini ya kodi, na kuimarisha ukuaji wa uchumi ili kuifanya Uingereza kuwa na ushindani mkubwa baada ya kujitoa kkatika Umoja wa Ulaya.”

“Natambua kwamba kulingana na hali ilivyo, siwezi kutekeleza kazi yangu ipasavyo kwa kulingana na ahadi nilizotoa na matarajio ya chama cha conservative. Kwa hivyo, nimezungumza na mfalme, na sasa natangaza kwamba najiuzulu kama kiongozi wa chama cha conservative.”

Kabla ya kujiuzulu, wabunge 17 walikuwa tayari wamesema kwamba wanamtaka Liz Truss kujiuzulu, na wabunge 100 walikuwa wameandika barua kwa kamati ya uongozi na mabadiliko ndani ya chama.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *