Handeni. Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amewataka wananchi waliohamia kijiji cha Msomera kutoka Ngorongoro wasiuze ardhi waliopewa na Serikali.
Waziri Nape amesema hayo leo Ijumaa Julai Mosi 2022 alipofanya ziara yake ya siku moja katika kijiji cha Msomera kwaajili ya kukagua miundombinu iliyojengwa na kuzungumza na wananchi hao.
Amesema kuhusu suala la hati za kumiliki ardhi, Serikali inalifanyia kazi kuliweka sawa kwa wenyeji na wageni na kama kutakuwa na tatizo basi Serikali itatua changamoto hiyo.
Ameongeza kuwa wananchi wenyeji walinde miundombinu yote ambayo inajengwa kwani Serikali inatumia pesa nyingi katika kuwawekea wananchi hao mazingira bora.
“Wale wanaopewa ardhi jizuieni kuuza hasa wakina baba maana watakuja watu wakitaka kununua kwa sababu kuna barabara, umeme na miundombinu mingine na mahali pakiwa na mawasiliano watu wanakimbilia, kwepeni kuuza ardhi mliopewa niahidi tutaongeza hizi huduma”, amesema Waziri Nape.
Diwani VIiti Maalumu kutoka Ngorongoro, Veronica Metruda amesema wananchi wa Ngorongoro wanatakiwa kuhasika kuhamia Msomera kwani fursa zipo nyingi kuliko Ngorongoro.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Siriel Mchembe kwa upande wake ameipongeza Serikali kwa kuweka mnara wa simu kwenye eneo hilo ambapo kwa sasa wananchi wanapata mawasiliano kupitia mtandao wa Airtel, kwani mawasiliano hayo yatasaidia pia suala la ulinzi.
Amesema wananchi kila mmoja anatakiwa kuwajibika kwenye hilo endapo ataona lolote ambalo linaweza kusababisha uvunjifu wa amani, atoe taarifa sehemu husika.
Zaidi ya kaya 67 tayari zimeshawasili katika kijiji cha Msomera kutoka Ngorongoro na kuhamia rasmi hapo pamoja na mifugo yao+