Waziri wa Sheria wa Afrika Kusini amesema kiongozi wa mapinduzi ya kupinga ubaguzi wa rangi nchini humo Shujaa Nelson Mandela “atakuwa anatabasamu kwenye kaburi lake” kutokana na uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ambayo iliamuru utawala wa Kizayuni wa Israel kuchukua hatua zote zinazohitajika kuzuia vitendo vya mauaji ya kimbari huko Gaza.
Ronald Lamola alitoa kauli hiyo Jumamosi baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kuiamuru Israel kuzuia vitendo vya mauaji ya halaiki ambavyo vimekuwa vikiendelea kwa zaidi ya siku 100 katika vita vikali vya Israel dhidi ya eneo hilo lililozingirwa.
“Tunaamini kwamba Rais wa zamani Mandela atakuwa anatabasamu katika kaburi lake kama mmoja wa watetezi wa Mkataba wa Mauaji ya Kimbari,” Lamola alisema kando ya mkutano wa chama tawala cha African National Congress (ANC) nje ya mji mkuu, Johannesburg.
Chama cha ANC, ambacho kwa muda mrefu kimetetea haki ya Palestina, kiliunga mkono uamuzi wa serikali kuwasilisha kesi katika mahakama ya Umoja wa Mataifa mwezi Disemba, ikiwataka majaji kuweka hatua za dharura kuamuru Israel kusitisha mara moja hujuma yake ya kikatili katika eneo hilo lililozingirwa.
Lamola alisema hatua ya Afrika Kusini kuipeleka Israel mbele ya ICJ ni kitendo cha ujasiri kilichochochewa na nia ya kutetea utaratibu wa dunia unaozingatia sheria.
“Ni ushindi kwa sheria ya kimataifa kwamba hakuwezi kuwa na ubaguzi katika sehemu yoyote ya dunia na Israel haiwezi kuachwa wakati inapuuza majukumu yake ya kimataifa,” aliongeza.
Mapema Jumamosi pia, Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini ilisifu kama “ushindi madhubuti” uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki kwamba Israel lazima ifanye kila iwezalo kuzuia vitendo vya mauaji ya kimbari huko Gaza.
“Huu ni ushindi madhubuti kwa utawala wa sheria wa kimataifa na hatua muhimu katika kutafuta haki kwa watu wa Palestina,” wizara hiyo ilisema katika taarifa.
Afrika Kusini imesema inatumai kwa dhati kwamba Israel itachukua hatua za kutekeleza amri hiyo ya ICJ.
Jana Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa aliapa kwamba nchi yake haitalegea katika ahadi yake kwa Wapalestina kupata haki yao ya kujitawala. Katika hotuba yake kwa taifa kwa njia ya televisheni muda mfupi baada ya hukumu ya ICJ Ramaphosa alisema anatumai agizo hilo litafungua njia ya kusitisha vita Gaza.
Ramaphosa alisema baadhi wameikosoa Afrika Kusini kwa kuipeleka Israel ICJ, lakini akasisitiza kuwa kama nchi iliyokumbwa na ubaguzi wa rangi, haiwezi kusimama na kutazama maovu yanayoendelea bila kuchukua hatua.