Waziri mmoja nchini Ethiopia ameutaja Ubalozi wa Marekani nchini Ethiopia kuwa ni wa ‘kigaidi’ na kwamba haupaswi kuwa nchini humo.
Faraan: Taye Dendea Aredo, Waziri wa Nchi wa Ethiopia, ameutuhumu ubalozi wa Marekani uliopo mjini Addis Ababa kuwa unachochea ghasia na kuhimiza ugaidi. Ameandika ujumbe huo katika ukurasa wake wa Facebook na kusisitiza kuwa haandiki kama waziri bali anaandika kama raia wa kawaida na kuongeza kuwa Ubalozi wa Marekani unachochea mivutano kwa kuleta hofu kupitia kutoa tahadhari za usalama.
Wiki iliyopita ubalozi wa Marekani ulionya kuhusu hatari ya shambulizi la kigaidi katika mji mkuu wa Ethiopia na maeneo mengine nchini humo. Pia umewaonya raia wa Marekani kuondoka nchini humo kutokana na kuongezeka ghasia wakati kundi la waasi wa Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF) likidaiwa kukaribia Addis Ababa. Serikali ya Ethiopia inakanusha vikali madai kuwa waasi wanakaribia kuuteka mji mkuu huo.
Aredo amesema Waethiopia hawataki kuona nchi yao ikigeuka kuwa Libya au Iraq ambazo Marekani ilizivamia kijeshi na kuangusha serikali na kuepelekea nchi hizo zitumbukie katika matatizo.
Ameongeza kuwa Ubalozi wa Marekani unapaswa kuondoka Ethiopia mara moja na hatua kwa hatua balozi zote za Marekani ziondoke Afrika.
Hivi karibuni Waethiopia katika maeneo mbali mbali duniani wameshiriki katika maandamano nje ya balozi za Marekani kulaani kile wanachosema ni uungaji mkono kwa waasi wanaotaka kuiangusha serikali ya nchi hiyo.