Waziri wa Mambo ya Nje wa Gabon afariki dunia ghafla kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri

Waziri wa Mambo ya Nje wa Gabon, Michael Moussa Adamo, amefariki dunia ghafla kwa mshtuko wa moyo wakati wa kikao cha Baraza la Mawaziri.

Taarifa rasmi ya serikali ya Gabon imethibitisha habari hiyo ya kufariki dunia Michael Moussa Adamo ambaye alikuwa mtu wa karibu na mshirika wa muda mrefu wa Rais Ali Bongo, hata kabla ya kuwa kwake rais mwaka 2009.

Taarifa zinasema kuwa, waziri huyo wa mambo ya nje wa Gabon amefariki dunia “licha ya juhudi za wataalamu” za kujaribu kuokoa maisha yake.

Duru moja ya Ikulu ya Gaboni imesema kwamba, Adamo alikuwa amekaa kitako mwanzoni mwa kikao cha Baraza la Mawaziri na ghafla akaanza kujisikia vibaya.”

Duru hiyo ambayo haikutaka kutajwa jina lake kwenye vyombo vya habari pia imsema, waziri huyo wa mambo ya nje wa Gaboni alipelekwa haraka kwenye hospitali ya kijeshi akiwa amepoteza fahamu na alifariki dunia baada ya saa sita mchana.

Rais Ali Bongo amemtaja Moussa Adamo kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba alikuwa “mwanadiplomasia mkubwa na mwanasiasa wa kweli”.

Katika ujumbe wake huo, Rais Bongo amesema: “Kwangu mimi, alikuwa, kwanza kabisa, rafiki, mwaminifu na mtiifu ambaye ningeweza kumtegemea muda wote.”

Wakati Bongo alipochaguliwa kuwa rais baada ya kifo cha babake Omar Bongo Ondimba mwaka wa 2009, Moussa Adamo aliwahi kuwa mshauri wake maalumu.

Alikuwa balozi wa Gabon nchini Marekani kwa muda wa muongo mmoja hadi mwaka 2020 na baadaye alikua waziri wa ulinzi na kisha waziri wa mambo ya nje kuanzia mwezi Machi mwaka jana.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *