Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo Jumatano ameelekea nchini Tanzania baada ya kumaliza ziara yake ya kikazi katika nchi ya Mali ya Magharibi mwa Afrika.
Hiyo ni ziara rasmi ya kwanza ya Hossein Amir-Abdollahian barani Afrika tangu ateuliwe kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran.
Aliwasili nchini Mali juzi Jumatatu na kufanya mazungumzo ya kina na viongozi wa nchi hiyo akiwemo mkuu wa serikali ya mpito ya nchi hiyo, Assimi Goita. Mazungumzo yake na Goita yamefanyika usiku wa kuamkia leo Jumatano kabla ya kuelekea nchini Tanzania.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema mwishoni mwa ziara yake nchini Mali kuwa, uhusiano wa miaka mingi na wa kale wenye misingi imara baina ya ustaarabu mkongwe wa Iran na ule wa Mali unalifanya kuwa la dharura suala la kuimarishwa uhusiano wa pande mbili katika nyuga zote na hasa kilimo.
Waziri Amir-Abdollahian pia amesema, ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni wa amani na ushirikiano katika nyuga zote pamoja na kuongezwa kazi za mashirika ya sayansi na tekonolojia ya Iran barani Afrika.
Kwa upande wake Kanali Assimi Goita, Kiongozi wa Serikali ya Mpito ya Mali ametaka kuimarishwa zaidi ushirikiano wa Bamako na Tehran katika nyuga za kiuchumi, kibiashara na kielimu na kueleza utayari wa nchi yake wa kuwa mwenyeji wa wenye viwanda na wanaharakati wa kiuchhumi.