Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran afanya mazungumzo na viongozi wakuu wa Oman

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekutana katika nyakati tofauti na Waziri wa Mambo ya Nje na Waziri wa Ofisi ya Mfalme wa Oman, wakajadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu masuala yenye maslahi kwa pande mbili.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ambaye alisafiri kuelekea Muscat Jumanne usiku, leo amekutana na kuzungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Seyyed Badr bin Hamad Albusaidi.
Amir-Abdollahian leo asubuhi pia amekutana na Jenerali wa Jeshi Sultan bin Mohammad Al Nu’mani, Waziri wa Ofisi ya Sultani wa Oman na kubadilishana mawazo kuhusu namna ya kupanuliwa na kustawishwa ushirikiano wa nchi mbili katika nyuga mbalimbali.
Mapema kabla ya hapo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alikutana na kufanya mazungumzo na Mfalme wa Oman Sultan Haitham bin Tariq Al Saeed na kumkabidhi ujumbe wa maandishi wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wenye mwaliko rasmi kwa Sultani wa Oman kuizuru Iran.

Katika mazungumzo yake na Mfalme wa Oman, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria masuala yenye maslahi ya pamoja kwa nchi mbili, na mbali na kutathmini mafanikio ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Seyed Ebrahim Raisi mjini Muscat, ametilia mkazo pia umuhimu wa kutekelezwa kikamilifu makubaliano yaliyofikiwa kati ya nchi mbili.

Amir Abdullahian amesisitizia pia kustawishwa katika pande zote uhusiano na ushirikiano kati ya nchi mbili katika nyanja za biashara, uchumi, nishati, utalii, uchukuzi na nyanja nyinginezo.
Kwa upande wake, Sultani wa Oman ameeleza matumaini aliyonayo ya kuitembelea Iran muda si mrefu ujao na kustawishwa zaidi na zaidi uhusiano kati ya Tehran na Muscat.
Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *