Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amekutana na kuzungumza na Sayyid Hassan Nasrallah” Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran (IRNA), katika kikao hicho kilichohudhuriwa na Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Lebanon Mojtaba Amani na ujumbe uliofuatana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian na Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon wamejadili matukio ya hivi punde katika eneo hilo, haswa kuhusu Lebanon na Palestina.
Kadhalika, katika mkutano huo, wawili hao wamebadilishana mawazo kuhusu vitisho vya utawala wa Kizayuni na kujiandaa kwa mhimili wa muqawama katika kukabiliana na matukio mapya ya kieneo na kimataifa.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesafiri nchini Lebanon kwa mwaliko wa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Lebanon kwa lengo la mashauriano ya pande mbili, ya kikanda na kimataifa na kujadili matukio ya hivi punde huko Palestina.
Amir-Abdollahian ameongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendelea kuunga mkono kwa dhati wananchi, serikali, jeshi na harakati ya Hizbullah ya Lebanon.
Aidha amesema Iran inatoa wito kwa mirengo yote ya kisiasa ya Lebanon kuendelea na mazungumzo na makubaliano kuelekea uchaguzi wa rais na kukamilika kwa mchakato wa kisiasa.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesisitiza kuwa: Mikondo tofauti ya kisiasa nchini Lebanon ndiyo itakayoamua rais mpya wa nchi hiyo kwa umahiri na bila ya uingiliaji wowote wa kigeni.
Wabunge wa Lebanon hadi sasa hawajafikia muafaka kuhusu uchaguzi wa mrithi wa “Michel Aoun” baada ya kumalizika kwa muhula wa miaka sita wa urais huyo, na kadhia hii imeibua wasi wasi kuhusu kushadidi mgogoro wa kisiasa nchini Lebanon.