Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iraq amesema kuwa nchi za Ulaya haziko tayari kuwarejesha nyumbani raia wa nchi hizo wanachama wa kundi la Daesh.
Daesh na makundi mengine ya kigaidi mwaka 2017 yalisambaratika na kushindwa baada ya miaka minne ya operesheni kubwa za kigaidi huko Syria na Iraq na baada ya kukalia kwa mabavu sehemu kubwa ya ardhi ya nchi hizi mbili. Hata hivyo, mabaki ya makundi hayo bado yanafanya operesheni za kigaidi katika nchi za Iraq na Syria dhidi ya raia na kushambulia askari usalama.
Fuad Hossein, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq amesema: Kuna takriban familia 70,000 za magaidi wa Daeh (ISIS) nchini Syria, ambao wanahesabiwa kuwa hatari kwa Iraq.
Ameongeza kuwa: “Ninaonya kwa mara nyingine tena juu ya hatari ya itikadi za ISIS, na itikadi hizo zipo katika sehemu ya jamii ya Iraq na Syria, na ikiwa magaidi hawa wataanza tena shughuli zao, watakuwa hatari kubwa.”
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq amesema: “Raia wa nchi 51 hadi 52 wako katika kambi ya al-Hol, ambayo inatumiwa kama kambi ya kutoa mafunzo kwa mujibu wa itikadi ya Daesh, na hata watoto waliokuwa na umri wa miaka 10 sasa wamefikia umri wa miaka 16 au 17 na wamepewa mafunzo kwa kuzingatia itikadi za ISIS.”
Fuad Hossein ameongeza kuwa: Hili si suala mahsusi kwa Iraq, kwa sababu magaidi hao wametoka katika nchi mbalimbali zikiwemo za Ulaya, lakini nchi hizo hazitoi ushirikiano wa kuwarejesha raia wao wanachama wa Daesh ambao wanahesabika kuwa ni hatari kwa jamii ya watu wa Iraq na Syria.
Kambi ya “Al Hol” iko katika mkoa wa Al-Hasaka kaskazini mashariki mwa Syria na karibu na mpaka wa nchi hiyo na Iraq, na inahifadhi zaidi ya watu 57,000 ambao wengi wao ni wanachama wa kundi la kigaidi la ISIS. Umoja wa Mataifa na taasisi nyingine kadhaa za kimataifa zimekuwa zikitahadharisha kuhusu hali mbaya inayotawala kambi ya Al-Hol.