Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Faisal bin Farhan ameelezea nia yake ya kukutana haraka na Waziri mwenzake wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian, baada ya nchi hizi mbili kufikia makubaliano ya kufufua uhusiano baina yao.
Akihojiwa na gazeti la Al-Sharq Al-Awsat, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia amesema: Makubaliano kati ya nchi yake na Iran ya kurejesha uhusiano wa kidiplomasia yanathibitisha nia ya kweli ya pande zote mbili ya kutatua hitilafu zao kwa njia ya mazungumzo.
Ameongeza kwa kusema: Tunajiandaa kurejesha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi zetu hizi mbili katika kipindi cha miezi miwili ijayo, na ni wazi kwamba tutakuwa na mikutano ya mara kwa mara katika siku zijazo.
Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia amesema katika sehemu moja ya mahojiano hayo kwamba, jambo muhimu zaidi katika mahusiano ya kimataifa ni kuweko uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi na nchi. Suala hilo linapokuja kwa nchi mbili kubwa na jirani za Saudi Arabia na Iran, linakuwa na umuhimu mkubwa zaidi. Nchi zetu zina mambo mengi ya pamoja ya kidini, kiutamaduni, kihistoria na mifungamano imara ya ustaarabu, hivyo uhusiano wa kidiplomasia kati yetu ni muhimu sana.
Ameongeza kuwa: “Makubaliano haya yalifikiwa kwa uungaji mkono na upatanishi wa China baada ya awamu kadhaa za mazungumzo katika miaka miwili iliyopita huko Iraq na Oman, na kwamba Saudi Arabia inaendelea na juhudi zake za kudumisha amani na kupunguza mivutano. Inaamini kuwa ni na jukumu lake kuimarisha usalama na utulivu kieneo na kimataifa.
Vile vile amesema, tunatarajia kufungua ukurasa mpya na Iran na kuboresha upeo wa ushirikiano ambao utakuwa na taathira chanya katika kuimarisha usalama na utulifu na kukuza maendeleo na ustawi, si tu katika nchi hizo mbili, bali pia katika eneo hili lote na dunia nzima kiujumla.