Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda akosoa kushindwa jamii ya kimataifa kutatua mgogoro wa Gaza

Jeje Odongo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda amesema anasikitishwa sana na kushindwa jamii ya kimataifa katika kutatua mgogoro wa Gaza wakati huu ambapo utawala haramu wa Israel unatekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa eneo hilo.

Akizungumza na Shirika la Habari la Anadolu katika Kongamano la Diplomasia la Antalya, Odongo ameelezea masikitiko yake kuhusu “mauaji na uharibifu unaoendelea” katika eneo hilo lililozingirwa.

Amesema: “Inasikitisha sana kwamba ulimwengu, hadi sasa, haujaweza kutekeleza majukumu na maamuzi yake kuhusu hali ya Gaza.”

Hali kadhalika amesema: “Kushindwa huku kwa dunia kunakatisha tamaa sana,” na kuongeza kuwa, kuna  udharura wa kamii ya kimataifa “kufanya kazi pamoja” ili kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Gaza.

Akielezea wasiwasi wake kuhusu hali ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, waziri huyo amesema: “Inasikitisha kwamba binadamu hawachukuliwi kama binadamu.”

Utawala wa Kizayuni kwa uungaji mkono wa pande zote wa Marekani na serikali za Ulaya waitifaki wa Washington, umekataa kuwajibika kuhusu jinai zake na hivyo kuendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya wananchi wasio na ulinzi huko Palestina.

Kufuatia operesheni ya kimbunga cha Al-Aqsa tarehe 7 Oktoba 2023, mashambulizi ya utawala wa Israel yameshtadi dhidi ya raia wa Palestina na miundombinu ya kiuchumi na afya, zikiwemo hospitali za eneo la Gaza.

Hadi sasa vita hivyo vya mauaji ya kimbari vimepelekea kuuawa Wapalestina wasiopungua 30,410, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na wengine 71,700 kujeruhiwa.

Serikali za Magharibi ambazo kila mara zimekuwa zikidai kuwa ni watetezi wa haki za binadamu, zimekaa kimya kuhusiana na matukio ya hivi karibuni huko Gaza na hali mbaya ya kibinadamu ya eneo hilo na kwa namna fulani kuhalalisha jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Palestina.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *