Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani (WFP) limetangaza kuwa, litalazimika kusitisha msaada muhimu wa kibinadamu kwa wakazi milioni moja wa jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji kutokana na ukata wa fedha.
Taarifa hiyo imeeza kuwa, shirika hilo litalazimika kusitisha utoaji misaada kwa raia hao endapo halitapokea fedha za nyongeza ifikapo kilele cha msimu wa njaa mwezi Februari mwakani kutokana na ukata wa fedha linaokabiliwa nao.
Antonella D’Aprile ambaye ni Mkurugenzi Mkazi wa WFP nchini Msumbiji ameziambia duru za habari kwamba Cabo Delgado ni jimbo la Msumbiji lisilo na uhakika wa chakula na uhakika wa chakula unadorora kila uchao, huku takribani watu milioni 1.15 jimboni humo wakiwa kwenye janga au udharura wa njaa, huku takwimu mpya zaidi zikionesha hali inaweza kuwa mbaya zaidi katika siku za usoni.
Wakati huo huo kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR huko Geneva Uswisi, wakazi wa jimbo hilo wameshuhudia madhila makubwa yakitendeka mbele ya macho yao ikiwa ni pamoja na wapendwa wao kuuawa, kukatwa vichwa, kubakwa, nyumba zao kubomolewa na miundombinu mingine kuchomwa moto, huku wanaume na wavulana wakilazimishwa kujiunga na vikundi vya wapiganaji wenye silaha.
Mashambulioi ya makundi ya kigaidi na kundi la kigaidi la Daesh huko Cabo Delgado yameua maelfu ya watu tangu mzozo ulipozuka mwaka wa 2017, na kuvuruga miradi ya mabilioni ya dola ya gesi asilia na uchimbaji madini.
Zaidi ya raia 800,000 wamekimbia makwao tangu mashambulizi ya kigaidi kuanza miaka tano iliyopita kaskazini mwa Msumbiji.