WHO: Mripuko wa nne wa Ebola katika jimbo la Equateur, DRC umetokomezwa

Shirika la Afya Duniani WHO limetangaza kuwa, mripuko wa Ebola uliotangazwa tarehe 23 mwezi Aprili mwaka huu huko Mbandaka, mji mkuu wa jimbo la Equateur katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umetokomezwa.

Taarifa iliyotolewa na WHO katika miji ya Kinshasa, DRC na Brazzaville, Jamhuri ya Kongo, imesema mripuko huo ulikuwa ni wa 3 kwa jimbo la Equateur tangu mwaka 2018 na wa 14 kwa nchi hiyo ya ukanda wa Maziwa Makuu barani Afrika.

Shirika la Afya Duniani limesema mafanikio ya kutokomeza ugonjwa huo yametokana na uzoefu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika kudhibiti Ebola, timu za kitaifa za kushughulikia dharura sambamba na usaidizi kutoka shirika hilo bila kusahau wadau na hatua za haraka zilivyochukuliwa mara baada ya kutangazwa kwa mripuko huo tarehe 23 mwezi Aprili mwaka huu.

Jumla ya wagonjwa wanne waliothibitishwa ndio waliofariki dunia pamoja na mtu mmoja aliyeshukiwa kuwa na ugonjwa huo, idadi ambayo WHO imesema ni  ndogo ikilinganishwa na miripuko ya awali, mathalani wa kuanzia mwezi Juni hadi Novemba 2020 ambapo kulikuwa na wagonjwa 130 waliothibitishwa na kati yao hao 55 walifariki dunia.

Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moeti, amesema wanapongeza na kutoa shukurani kwa hatua bora na za haraka zilizochukuliwa na mamlaka za kitaifa, ambazo zimepelekea mripuko wa mara kutokomezwa haraka na maambukizi kutokuwa makubwa.

Hadi sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekuwa na miripuko 14 ya Ebola tangu mwaka 1976, ambapo kati ya hiyo, sita imekumba nchi hiyo tangu mwaka 2018.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *