WHO: Umri wa mtu kuishi, tena akiwa na afya Afrika umeongezeka

Shirika la Afya Duniani, WHO limesema umri wa mtu kuishi barani Afrika, tena akiwa na afya bora umeongezeka kwa wastani wa miaka 10 kwa mtu mmoja kati ya mwaka 2000 na 2019, ikiwa ni ongezeko kubwa kuliko ukanda mwingine wa shirika hilo duniani katika kipindi hicho hicho; na sababu ni pamoja na kuimarika huduma za mama na mtoto.

Taarifa iliyotolewa na WHO kanda ya Afrika katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kongo, Brazzaville imenukuu ripoti ya mwaka huu ya kufuatilia huduma ya afya kwa wote kanda ya Afrika, ambayo hata hivyo imetahadharisha kuwa ugonjwa wa Covid-19 unaweza kutibua mafanikio hayo.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa, idadi ya miaka ambayo mtu anaishi akiwa na afya njema barani Afrika imeongezeka hadi umri wa miaka 56 mwaka 2019 kutoka umri wa miaka 46 mwaka 2000.

Taarifa hiyo ya WHO imefafanua kwa kusema: ingawa bado tuko nyuma ya wastani wa Dunia wa umri wa kuishi wa miaka 64, bado katika kipindi hicho hicho, wastani wa kuishi duniani uliongezeka kwa miaka mitano pekee.

Shirika la Afya Duniani limeendelea kueleza katika taarifa yake kwamba, kuimarika kwa huduma za msingi za afya, mafanikio katika afya ya uzazi hasa kwa wajawazito, watoto wachanga na afya ya mtoto na vilevile maendeleo mazuri katika kudhibiti magonjwa ya kuambukiza kama vile UKIMWI, Kifua Kikuu na  Malaria ni masuala yaliyochangia kuongezeka umri wa kuishi kwa mtu mmoja barani Afrika.

Akizungumzia mafanikio hayo, Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika, Dkt. Matshidiso Moeti amesema huo ni ushahidi wa harakati za bara hilo kuboresha afya na ustawi wa wakazi wake.

“Ina maana watu wengi wanaishi maisha yenye afya, wanaishi muda mrefu na wachache wanatishiwa na magonjwa ya kuambukiza na wana huduma bora za kujikinga na magonjwa,” amesema Dkt. Moeti.

Hata hivyo ameonya kuwa, maendeleo hayo yasikome kwa kuwa bila hatua za kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile saratani au kansa, mafanikio yaliyopatikana yatatoweka.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *