WHO: Watu milioni 24 wanaishi na ugonjwa wa kisukari barani Afrika

Wakati jana Jumatatu ulimwengu uliadhimisha siku ya kisukari duniani, bara la Afrika linaonekana kuwa na changamoto kubwa ya ugonjwa huo kwa mujibu wa takwimu mpya za Shirika la Afya la Duniani (WHO).

Maadhimisho hayo yanayofanyika kila mwaka kwa lengo la kuelimisha umma kuhusu ongezeko la mzigo wa ugonjwa huo na mikakati ya kuzuia na kudhibiti tishio lake yamekwenda  sambamba na kuweko uwezekano wa kuongezeka pakubwa ugonjwa wa kisukari duniani katika miaka ijayo.

Takwimu zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku ya kisukari duniani zinaonyesha kiwango cha changamoto ya ugonjwa wa kisukari Afrika ni kikubwa ambapo watu wazima milioni 24 hivi sasa wanaishi na ugonjwa wa kisukari na idadi inatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 129% hadi kufikia watu million 55 ifikapo mwaka 2045.

Dkt. Matshidiso Moeti Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika amesema kuwa, “Mwaka watu 416,000 waliaga dunia kwa ugonjwa wa kisukari barai Afrika na kwamba, ugonjwa huo unatarajiwa kuwa miongoni mwa vyanzo vikuu vya vifo Afrika ifikapo mwaka 2030.

Mkurugenzi huyo wa WHO Kanda ya Afrika anasema, changamoto kubwa katika juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo ni ukweli kwamba zaidi ya mtu 1 kati ya kila watu 2 barani Afrika anayeishi na kisukari hajawahi kupimwa, hivyo kuongeza fursa za nyenzo za upimaji na dawa kama insulini, ni moja ya maeneo yanayopaswa kufanyiwa kazi haraka.”

Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema idadi kubwa ya wagonjwa wa kisukari hawapati dawa aina ya insulini ambayo ni muhimu katika kupunguza makali ya ugonjwa huo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *