Wimbi jipya la mauaji ya wasomi na wanaharakati laripotiwa Saudia

Wimbi jipya la kunyongwa na kuuliwa wasomi na wanaharakati wa masuala ya kijamii limeripotiwa nchini Saudi Arabia baada ya utawala wa kifalme wa nchi hiyo kumtia nguvuni mwanazuoni wa Kiislamu katika mji mtakatifu wa Madina.

Kamata kamata hiyo nchini Saudia inafanyika kwa mujibu wa sheria eti za kukabiliana na ugaidi na sheria nyingine zilizowekwa kwa ajili ya kuhalalisha uhalifu wa utawala wa kifalme dhidi ya wapinzani na watetezi wa haki za binadamu.

Mashirika ya habari yameripoti kuwa, vyombo vya usalama vya Saudi Arabia vimemtia nguvuni Sheikh Kadhim al Amri, mtoto wa Ayatullah Muhammad al Amri katika mji mtakatifu wa Madina. Msomi huyo ameungana na watoto wake wawili, Muhammad na Rajai ambao walikamatwa na vyombo vya usalama na kufungwa gerezani mwezi Aprili mwaka huu.

Utawala wa Saudi Arabia pia umetumia sheria hizo kuwahukumu kifo Muhammad Aal Tahnun, Mustafa Abu Shaheen na Abdullah al Qazwini, na Shirika la kutetea haki za binadamu nchini Saudi Arabia limetangaza kuwa, raia wengine 59 wanakabiliwa na hatari ya kunyongwa nchini Saudi Arabia.

Maafisa wa serikali ya Saudi Arabia bado hawajachapisha takwimu rasmi kuhusu idadi ya wafungwa wa kisiasa na wa haki za binadamu wanaoshikiliwa katika jela za nchi hiyo. Hata hivyo kwa mujibu wa mtandao wa habari ya The Middle East, mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yameripoti kuwa idadi ya wafungwa wa kisiasa nchini Saudi Arabia ni karibu watu 30,000, ambao wako katika mazingira magumu, yakiwemo mateso ya kila aina na udhalilishaji.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *