Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, nchi kadhaa za Ulaya zimetuma maoni yao ya kutaka kuuziwa ndege zisizo na rubani za Iran.
Shirika la habari la Tasnim limemnukuu Kamanda Reza Talaei-Nik akisema hayo na kuongeza kuwa: “Hivi sasa kuna maombi mengi ya nchi zinazotaka kununua ndege zetu zisizo na rubani na tumepokea maombi kadhaa pia kutoka kwa nchi za Magharibi na Ulaya ambazo tab’an hazitaki kutajwa majina.“
Kamanda Talaei-Nik ambaye ni Naibu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Usimamizi na Mpango Mkakati na pia ni Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Iran amesema katika mahojiano aliyofanyiwa na mwandishi wa shirika la habari la Tasnim kwamba Iran iko tayari kuziuzia nchi rafiki, droni na ndege zake zisizo na rubani tab’an kwa masharti maalumu yakiwemo ya kutotumika ndege hizo katika masuala yaliyoko nje ya makubaliano.
Akizungumzia maonesho ya mafanikio ya sekta ya ulinzi ya Iran Kamanda Talaei-Nik amesema: “Tuna maonyesho ya kudumu na ya nje ya nchi ya kuwaonesha walimwengu mafanikio yetu ya kiulinzi, na bila shaka, si zana zetu zote zinaoneshwa kwenye maonyesho hayo. Baadhi ya mafanikio yetu hayako kwenye “kikapu” cha kuuza bidhaa zetu kwa sababu maalumu.”
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Iran ameongeza kuwa, jeshi linalotumia silaha au droni na ndege zisizo na rubani, lazima lipitie mchakato unaohitajika wa mafunzo ya silaha hizo na kuongeza kuwa, mikataba na makubaliano na pande mbalimbali lazima yafayike ndani ya mfumo wa masuala ya kisheria na ya kimataifa.