Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) kimemchagua Xi Jinping kuendelea kuwa katibu wake mkuu kwa muhula wa tatu katika kikao kilichomalizika jana na hivyo kumuidhinisha kuendelea kuwa rais wa China.
Kikao cha 20 cha Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China kimefanyika mapema leo chini ya uwenyekiti wa Xi. Wanachama pia walimchakuwa Xi kuwa mwenyekiti wa Tume Kuu ya Kijeshi ya CPC.
Katika Kongamano la 20 la Kitaifa la CPC, washiriki waliidhinisha mpango mpya wa ustawi wa China wakati huu ambao dunia inakabiliwa na mgororo wa kiuchumi. Akihutubu katika kikao hicho, Xi amesema China itaharakisha uanzishwaji wa mpango mpya wa maendeleo ya kiwano cha juu. Aidha amesema China itaendeleza mabadiliko katika mfumo wa kiuchumi wa kisochialisti huku akisisitiza kuwepo uhusiano zaidi wa kiuchumi na nchi zingine duniani.
Xi amesema, China inafuata sera za diplomasia ya amani ya kujitawala na kujiamulia mambo. Ameongeza kuwa siku zote China inalinda kanuni za kimsingi za uhusiano wa kimataifa na haki duniani, na inapinga ubabe na siasa za mabavu. Amesisitiza kuwa, China haitatumia mabavu wala haitavamia nchi nyingine.
Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, China imekuwa ikishikilia asilimia 18.5 ya uchumi wa dunia na mshirika mkubwa wa kibiashara wa zaidi ya nchi 140 duniani.
Wakati huo huo duru zinadokeza kuwa mkuu wa chama cha kikomunisti huko Shanghari, Li Qaing, ambaye aliandamana na Xi alipofika katika ukumbi wa mkutano yamkini akachukua nafasi ya Waziri Mkuu wa China wakati waziri mkuu wa sasa Li Keqiang atakapostaafu mwezi Machi mwakani.