Msemaji wa vikosi vya ulinzi vya Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo vinao uwezo wa kujibu mapigo dhidi ya shambulio lolote lile.
Brigedia Saree ameeleza katika taarifa: “huko nyuma, maadui walikuwa wakishambulia Sana’a na mikoa mingine kwa mabomu na makombora bila kujibiwa; lakini leo tunao uwezo wa kujibu shambulio lolote lile kwa makombora kadhaa na ndege zisizo na rubani; na vikosi vyetu vya ulinzi vimefanikiwa kuweka hali ya mlingano ya kutoa kitisho na kumtia hofu adui.
Msemaji wa vikosi vya ulinzi vya Yemen ameongezea kwa kusema: “mlingano wa hivi karibuni ambao vikosi vyetu vya ulinzi vimeuweka katika kutekeleza majukumu yake ya kulinda rasilimali za mamlaka ya nchi kama mafuta na gesi ya Yemen, umethibitisha uwezo wa Yemen wa kuzuia uanzishwaji wa hujuma dhidi yake na pia upeo wa juu wa nguvu na uwezo vilionao vikosi vya ulinzi wa kulinda mamlaka ya kujitawala na rasilimali za nchi hii”.
Tangu Machi 2015, Saudi Arabia, ilianzisha mashambulizi makubwa ya kijeshi dhidi ya Yemen – nchi maskini zaidi ya Kiarabu – kupitia muungano wa nchi kadhaa za Kiarabu, ikiwemo Imarati, na kwa uungaji mkono na baraka kamili za Marekani na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.
Lakini baada ya miaka saba ya uvamizi dhidi ya Yemen na licha ya kuua maelfu ya watu na kuharibu miundombinu ya nchi hiyo, nchi hizo sio tu hazijafikia malengo yao, lakini pia zimelazimika kukubali kusitisha mapigano baada ya kuandamwa na vipigo vikali vya makombora na ndege zisizo na rubani za jeshi la Yemen vilivyolenga hadi ndani kabisa ya ardhi zao.