Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) limetangaza kuwa, asilimia 95 ya wananchi wa Afghanistan hawana chakula cha kutosha.
Taarifa yay Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) kanda ya Asia-Pasific imeeleza kwamba, katika miezi ya hivi karibuni hali ya kibinadamu nchini Afghanistn imezidi kuwa mbaya na kwamba, idadi ya watu wanaokabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula inazidi kuongezeka siku baada ya siku.
Umasikini, njaa na ukame ni mambo ambayo yamewafanya maisha ya wananchi wa Afghaistan kuwa magumu hasa katika kipindi hiki cha msimu wa baridi.
Katika miezi ya hivi karibuni asasi mbalimbali za kimataifa za utoaji misaada zimekuwa zikitahadharisha kuhusiana na kuzidi kuwa mbaya hali ya kibinadamu katika nchi hiyo hasa kutokana na uhaba mkubwa wa chakula unaowakabili wananchi wa nchi hiyo.
Kitambo kidogo nyuma, Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) lilikuwa limetangaza kuwa, ili kuzuia kutokea maafa ya kibinadamu nchini Afghanistan kuna haja kwa nchi hiyo kupatiwa misaada ya kibinadamu haraka iwezekanavyo.
Ripoti mbalimbali za kieneo na kimataifa zinaonyesha kuwa, kukosekana misaada ya kimataifa sambamba na ukame ulioambatana na kupanda pakubwa bei za bidhaa hasa vyakula, ni mambo ambayo yameifanya Afghanistan ijongewe na baa kubwa la njaa na kuitumbukiza nchi hiyo katika mgogoro na matatizo makubwa ya ukosefu wa chakula.