Zaidi ya wanamgambo 200 wa kundi la wanamgambo wa al-Shabab wameangamizwa nchini Somalia kufuatia operesheni ya kijeshi ya jeshi la nchini hiyo.
Taarifa ya jeshi la Somalia imethibitisha kutokea mauaji hayo dhidi ya wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabab na kueleza kwamba, operesheni hiyo ya jeshi imetekelezwa katika mji wa Galguduud.
Miongoni mwa waliouawa wamo makamanda wa ngazi za juu wa kundi hilo la kigaidi, imeeleza taarifa hiyo.
Gazeti la al-Ahram limeandika kuwa, mbali na jeshi la Somalia kuua makumi ya wanagambo wa al-Shabab katika shambulio hilo, limefanikiwa pia kutegua mabomu kadhaa yaliyokuwa yametegwa na wanamgambo hao.
Siku chache zilizopita pia watu wasiopungua 14 walipoteza maisha baada ya gaidi aliyekuwa amejifunga bomu kujiripua katika eneo lenye shughuli nyingi katikati mwa Somalia.
Kundi la kigaidi la al Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida limetangaza kuhusika na hujuma hiyo.
Kundi hilo la kigaidi linafanya hujuma hizo huku Somalia ikijiandaa kwa uchaguzi wa rais ulioakhirishwa mara kadhaa.
Tangu mwaka 2007, kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa al Qaida limekuwa likifanya mashambulizi ndani ya Somalia kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya nchi hiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.