Zaidi ya watoto milioni 3.5 wa Kenya kukosa skuli mwezi Januari kutokana na ukame

Shirika la misaada ya kibinadamu la Save the Children limetoa taarifa na kusema kuwa, zaidi ya watoto milioni 3.5 wa Kenya hawataweza kujiandikisha shuleni wakati masomo yatakapoanza mwezi Januari 2023 kutokana na ukame wa kupindukia.

Katika taarifa yake ya jana Jumanne, shirika hilo limesema, utafiti wake unaoesha kuwa, ukame unazidi kuwa mbaya na watoto wengi zaidi wenye umri wa kwenda skuli wanalazimila kuacha shule kutokana na ukame ambao Kenya inasema ni mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika miaka 40 iliyopita.

Yvonne Arunga, mkurugenzi wa shirika la Save the Children katika nchi za Kenya na Madagascar ameongeza kuwa: “Watoto ndiyo makundi yaliyoko hatarini zaidi na kwa kawaida ndio wanaothirika zaidi katika matukio ya dharura kama haya. Wazazi wanalazimika kuhama na watoto wao kutafuta chakula, malisho na maji kwa mifugo yao. Hii inahatarisha pia kupatikana mahitaji ya kimsingi kama vile chakula, maji safi, huduma za afya, na elimu kwa watoto hao.

Shirika hilo la kimataifa la misaada ya kibindamu limebainisha kuwa, hali imezidi kuwa mbaya walioathiriwa na ukame ni wafugaji wa kuhamahama ambao wamepoteza maelfu ya mifugo yao kutokana na ukosefu wa maeneo ya kulishia wanyama wao.

Shirika la Save the Children pia limeitaka serikali ya Kenya kuhakikisha kuwa skuli zinakuwa na maji ya kutosha ya kunywa, usafi wa mazingira na usafi wa watu binafsi wakati wa ukame ili kuboresha mazingira ya shule na kuwahimiza wanafunzi kuendelea na masomo.

Ripoti zinasema kuwa watu milioni 4.35 nchini Kenya wanakabiliwa na viwango vya juu vya uhaba wa chakula. Ripoti ya Mamlaka ya Taifa ya Kukabiliana na Majanga nchini Kenya inaonesha kuwa, huku skuli zikitarajiwa kufunguliwa mwezi Januari 2023, watoto wengine milioni 1.6 wako katika hatari kubwa ya kuacha shule.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *