Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amesisitiza kuwa, vijana wa kambi ya muqawama wanapaswa kusimama imara kukabiliana na madola ya kiistikbari kama ambavyo pia amewataka Waislamu kutumia njia zote zinazowezekana, kuhakikisha fikra za shahidi Qassem Soleimani zinabakia hai.
Sheikh Ibrahim Zakzaky amesema hayo katika mahojiano na shirika la habari la FARS kwa mnasaba wa mwaka wa watu tangu alipouawa shahidi, Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) na kuhimiza kuendelezwa njia ya shahidi huyo mkubwa.
Amesisitiza kuwa, ni wajibu kwa kila Muislamu huru kuendeleza njia na fikra za shahidi huyo na kutoruhusu jihadi yake kubwa kusahauliwa hata kidogo.
Aidha ametoa nasaha kwa vijana wa kambi ya muqawama akiwaambia: Vijana wanamuqawama wana jukumu na wajibu wa kusimama kidete kupambana na nchi za kibeberu kwani hiyo ndiyo njia pekee ya kuweza kuwakomboa wananchi kutoka kwenye makucha ya madola hayo ya kiistikbari.
Mwaka jana pia na wakati wa kumbukumbu ya mwaka wa pili wa kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Sheikh Ibrahim Zakzaky alitoa ujumbe maalumu na kukipa pole Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH.
Katika ujumbe wake huo wa mwaka jana, Sheikh Zakzaky alisema kuwa, Luteni Jenerali Qassem Soleimani alikuwa mwanastratijia wa aina yake ambaye alifanikiwa kusambaratisha njama zote za maadui hasa katika nchi za Iraq na Syria.
Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, aliuawa shahidi Januari 3, 2020 katika shambulio la anga lililofanywa na jeshi vamizi na la kigaidi la Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad, akiwa pamoja na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Mkuu wa harakati ya kujitolea ya wananchi wa Iraq ya al Hashd al Sha’abi na wanamapambano wengine wanane, wakati alipoelekea Iraq kwa mwaliko rasmi wa serikali ya nchi hiyo.