Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina amesisitiza kuwa, katu wananchi wa Palestina hawatasalimu amri mbele ya adui Mzayuni na kwamba, bendera ya Palestina itaendelea kupepea.
Ziyad al-Nakhala, Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina amebainisha kuwa, lengo la adui ni kutufanya watumwa hivyo katu hatuwezi kusalimu amri.
Kiongozi huyo mwandamizi wa Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina ameongeza kusema kuwa, adui ameligeuza eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kuwa makazi makubwa ya walowezi wa Kiyahudi ambao wamekuwa wakifanya mauaji na ugaidi dhidi ya Wapalestina.
Aidha amesema kama ninavyomnukuu: Anachokitaka adui ni kusambaratisha umoja wetu na kisha kutufanya watumwa; na hayo yote yanatokana na kuwa tunapinga madhila na uvamizi wa utawala ghasibu wa Israel.
Ziyad al-Nakhala amesema pia, inasikitisha kuwa baadhi ya Waarabu hawataki kusikia jina la Palestina, lakini jina la Palestina na taifa la Palestina vinazidi kukua siku baada ya siku.
Kadhalika amebainisha kwamba, Jihadul-Islami na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ni makundi ya muqawama ambayo yapo chini ya bendera moja ya Palestina na yapo katika vita vimoja na adui.
Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina amesema pia kuwa, wanaishukuru Iran, Syria, Qatar, Yemen, Lebanon na Misri, kama ambavyo wanamshukuru Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon na kwamba, wako pamoja na wafungwa wa Kipalestina katika mapambano yao.